Babati. Waliokuwa madiwani wa viti maalumu baraza lililopita, katika halmashauri ya mji wa Babati na Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wameshindwa kutetea nafasi zao.
Katika uchaguzi wa madiwani viti maalumu mjini Babati uliofanyika jana Julai 20, 2025 na kusimamiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) mkoa wa Manyara, Inyasi Amsi umekamilika huku vigogo wawili wa baraza lililopita wakiangukia pua.
Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Babati mjini, Eva Makilagi aliongoza tarafa ya Babati kwa kura 400, akifuatiwa na Katibu Mwenezi CCM Babati mjini, Salome Masasi (341) huku diwani wa baraza lililopita, Zainab Sige akiwa watatu kwa kupata kura (220).
Katika tarafa ya Gorowa, Rose Fraten aliongoza kwa kura 357 huku diwani wa baraza lililopita aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, Aziza Kambi akipata kura 175 na Sofia Songoro kura 53.
Hata hivyo, Amsi amesema uchaguzi huo ni mchakato hivyo hakuna mshindi ila wasubirie vikao vya ngazi ya juu vyenye mamlaka ya uteuzi.
“Pia wana CCM mnapaswa mtafute kura nyingi na za kishindo za mgombea urais Samia Suluhu Hassan ili viti maalumu viwe vya kutosha katika ngazi ya udiwani na ubunge,” amesema Amsi.
Kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, madiwani wawili wameshindwa kutetea nafasi zao.
Madiwani hao ni wa tarafa ya Naberera, Bahati Patson na tarafa ya Emboreet, Namnyaki Edward baada ya kuzidiwa kura na wenzao.
Patson ameangushwa na Rehema Abraham, huku Namyaki akiangushwa na Rehema Yohana.
Katika uchaguzi huo Rehema alipata kura 137, Paulina Ngenyai (94) Namnyaki (89) na Naomi Kuya (82).
Madiwani waliokuwa wanatetea nafasi zao Paulina Makeseni (Moipo), Neema Sinjori (Msitu wa Tembo), Rehema Laizer (Ruvu Remit) na Mwanjaa Jacob (Terrat) walifanikiwa kusalia katika kinyang’anyiro hicho.