Bao la Mzize bado lamliza Chalamanda

KIPA wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda amekiri licha ya kufungwa mabao kibao msimu uliopita, lakini bado anateswa na lile alilotunguliwa na straika wa Yanga, Clement Mzize na ndilo lililokuwa bora kufungwa na lilimshangaza na kumuuzia hadi leo.

Chalamanda ambaye ameitumikia Kagera kwa miaka minane mfululizo, ni miongoni mwa makipa wanaoongoza kwa kuokoa akifanya hivyo mara 56 akishika nafasi ya pili na wa kwanza ni Yona Amosi.

Akizungumza na Mwanaspoti Chalamanda alisema, Mzize ndiye mshambuliaji ambaye amemuachia historia ya kumfunga bao la tofauti, huku akimsifu ni mmoja wa mastaa wenye viwango vikubwa.

“Ile mechi ya kwanza ya msimu dhidi ya Yanga tulifungwa 2-0, lilianza bao la kwanza la Maxi Nzengeli, nikajua tumemaliza hapa, ila goli lake lilinishangaza sana,” alisema Chalamanda na kuongeza;

“Hiyo mechi tulikuwa nyumbani nakumbuka, alifunga bao la pili lililonishangaza ila makosa yalikuwa kwangu na mabeki wangu ila Mzize akatumia nafasi.”

Mzize ni miongoni mwa mastaa wanaofanya vizuri Ligi Kuu Bara akimaliza na mabao 14, huu ukiwa ni msimu wake wa tatu Yanga.

Mwanaspoti iliwahi kuandika JKT Tanzania ilikuwa imefikia pazuri kumnasa kipa huyo ikipanga kumpa mkataba wa miaka miwili kuitimikia timu hiyo ya jeshi.

“Chalamanda ni mmoja wa makipa waliofanya vizuri msimu uliomalizika, bila kujali hatua ya timu yake kushuka daraja,” alisema bosi huyo wa JKT.

Kagera ni moja ya timu mbili zilizoshuka daraja kwenda Ligi ya Championship ikiwa sambamba na KenGold baada ya kumaliza nafasi mbili za mwisho za msimamo wa Ligi Kuu iliyomalizika mwezi uliopita na kushuhudiwa Yanga ikitetea taji kwa msimu wa nne mfululizo.