Dodoma. Serikali ya Canada imetangaza ufadhili kwenye miradi mitatu yenye thamani ya Sh90 bilioni (sawa na Dola za Marekani milioni 32), ikihusisha kuboresha lishe shuleni kwa wanafunzi 65,000 wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Miradi mingine ni wa kuwanganisha vijana na fursa za kiuchumi unaojulikana kama mradi wa Bloom Afrika, kuwawezesha wanawake na wasichana waliopo pembezoni kupita mafunzo ya ujuzi.
Akizungumza leo Jumatatu, Julai 21, 2025 jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Randeep Sarai amesema mradi wa Bloom Afrika utakaogharimu karibu Sh50 bilioni (Dola za Marekani milioni 20) umelenga kujenga fursa na uongozi kwa wasichana na wanawake vijana hususan waliopo pembezoni.
Amesema mradi huo utanufaisha vijana 25,200 kutoka nchi za Tanzania, Rwanda na Somalia na umelenga kuwawezesha wanawake na wasichana kiuchumi kupitia ushirikishwaji wa kifedha na ujasiriamali.
Amesema nchini Tanzania mradi utanufaisha moja kwa moja vijana 3,500 na kwa njia isiyo ya moja kwa moja utawagusa watu wapatao 100,000, wakiwemo wazazi na walezi, wanajamii, taasisi za mafunzo ya ufundi stadi (TVET), taasisi za fedha ndogondogo, pamoja na mashirika yanayoongozwa na vijana na wanawake katika jamii, hasa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Ushirikiano huu siyo tu kuhusu mafunzo, bali kufungua uwezo na kubadilisha fursa kuwa matokeo chanya na tunawapatia vijana ujuzi na ujasiri wa kuunda maisha yao ya baadaye,” amesema.
Sarai amesema mradi wa pili ni kupitisha Shirika la Finca ambao utawaunganisha vijana na fursa na mafunzo ya ujuzi, uatamizi, biashara na mitaji na ukiwanufaisha vijana 41,000 wa nchi za Tanzania na Uganda hususan wasichana walio pembezoni.
“Wasichana wa Tanzania wapo hatarini kuacha masomo mapema, hivyo kwa mradi huo utasaidia kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaosaidia kuingia kwenye soko la ajira, kuongeza kipato na kupambana na umaskini,” amesema.
Amesema mradi wa pili utagharimu karibu Sh30 bilioni (Dola za Marekani milioni 12) ambao utasaidia kuunga mkono mkakati wa Serikali ya Tanzania wa lishe mashuleni ukihusisha watoto 65,000 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Amesema utasaidia katika kuimarisha lishe na kutokomeza utapiamlo.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameishukuru Serikali ya Canada kwa kuwekeza katika elimu ya ualimu ambayo ni nguzo muhimu ya kuhakikisha ujifunzaji bora katika shule.
“Juhudi hizi zinaonyesha dhamira ya dhati na endelevu ya Canada katika kukuza maendeleo ya rasilimali watu na ujumuishaji wa kijamii,”amesema Profesa Mkenda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Finca Canada, Drew Boshell amesema kupitia mpango wa ushirikiano wa kibiashara, vijana watapata ushauri kutoka kwa wajasiriamali waliobobea ambao watawapatia uzoefu wa moja kwa moja wa biashara kupitia mafunzo kwa vitendo.
Amesema vijana hao wataungwa mkono ipasavyo ili kuelewa soko la ajira.
“Cha muhimu zaidi, tumejikita katika kutoa huduma na bidhaa za kifedha zinazowafikia vijana popote walipo. Hii inajumuisha kupanua matumizi ya zana za benki za kidijitali, kutumia mawakala wa benki, na kutoa elimu ya kifedha ili vijana waweze kudhibiti fedha zao kwa ujasiri na kukuza biashara zao,”amesema.
Amesema matokeo ya mradi huo, zaidi ya vijana 40,000 watanufaika huku zaidi ya ajira 20,000 zikitarajiwa kuundwa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa programu bora na mikakati wa World Vision Tanzania (WVT), Simon Moikan amesema World Vision Tanzania mradi mpya wa Bloom Africa ni ahadi kwa wasichana na wanawake walioko pembezoni ambao ndoto zao zina thamani na sauti zao ni muhimu.
“Kwa msaada wa Serikali ya Canada, Serikali ya Tanzania na wadau wetu, tunapanda mbegu za matumaini zitakazochanua kuwa matokeo ya kudumu kwa vizazi vijavyo,”amesema.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja la Umoja wa Mataifa (WFP), Ronald Tran Ba Huy amesema mradi wa lishe mashuleni ni wa miaka mitano na utanufaisha watoto wa kike na wa kiume 65,000 katika mikoa ya Mtwara na Lindi.
“Huu ni uwekezaji katika rasilimali watu na ni hatua muhimu kuelekea kujenga kizazi kilichosoma, chenye afya na ustawi, kitakachochangia maendeleo ya Taifa kuelekea Dira ya 2050,”amesema.
Amesema pamoja na Tanzania kupiga hatua kubwa katika kuimarisha mpango wa lishe shuleni, bado inakabiliwa na changamoto ya mzigo wa utapiamlo hivyo juhudi hizo zinakwenda kusaidia kuupunguza mzigo huo.
“WFP inajivunia kusimama na Serikali ya Tanzania kuendelea kuwekeza mahali penye umuhimu mkubwa zaidi kwenye akili, afya na mustakabali wa watoto wetu,” amesema.