Doha. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kundi la waasi la M23 hatimaye wamefikia makubaliano ya awali ya amani yaliyotiwa saini katika mji wa Doha, Qatar mwishoni mwa wiki.
Azimio hilo, linalojulikana kama Declaration of Principles, linabeba matumaini mapya ya kufungua ukurasa wa mazungumzo ya kisiasa baina ya pande hizo mbili ambazo zimekuwa kwenye vita vya muda mrefu, hasa katika eneo la Mashariki mwa DRC.
Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na serikali ya Qatar kwa kushirikiana na Marekani na Umoja wa Afrika, yanahusisha kusitisha mapigano mara moja, kufungua njia ya mazungumzo ya kina na kuweka msingi wa kufikia makubaliano ya kudumu kabla ya Agosti 18 mwaka huu.
Azimio hilo la kanuni, limeweka misingi mikuu mitatu ya utekelezwaji wake likisisitiza kukoma mara moja kwa mapigano yaliyodumu mashariki mwa nchi hiyo, kushushwa kwa silaha zote ifikapo Julai 29, 2025 na kutathmini hali ya uimarishwaji wa usalama ifikapo Agosti 18.
Azimio hilo limeweka misingi ya kurejesha mamlaka ya serikali katika miji iliyokuwa imetekwa na kikundi cha waasi hao ikiwemo Kivu na Goma.
Katika azimio hilo, serikali ya DRC kupitia msemaji wake, Patrick Muyaya ilieleza kuwa pamoja na kutiwa saini kwa azimio hilo, bado msimamo wake kuhusu uondokaji wa waasi wa M23 katika maeneo wanayoyadhibiti uko palepale.
Muyaya alisema serikali haitakubali kujadili uwepo wa waasi katika ardhi ya DRC kwa namna yoyote ile. Akisisitiza kuwa mamlaka ya serikali lazima irejeshwe kwenye maeneo yote.
Kwa upande mwingine, viongozi wa M23 walitoa kauli ya kuridhia makubaliano hayo lakini wakaweka wazi lengo lao ni kuhakikisha haki, usawa na maendeleo yanarejea Mashariki mwa Congo. Msemaji wa kundi hilo, Lawrence Kanyuka alisema kuwa wao ni sehemu ya jamii ya Congo na hawatakubali kunyanyaswa au kufukuzwa kwa nguvu bila suluhisho la kisiasa linaloheshimu matakwa ya watu wa maeneo hayo.
Kiongozi mwingine wa kundi hilo, Bertrand Bisimwa, alinukuliwa akisema azimio hilo ni mwanzo wa kurejesha heshima kwa watu wa Congo waliokumbwa na madhila ya vita kwa muda mrefu. Alisisitiza kuwa M23 haiko kwenye mchakato huu kwa sababu ya kushindwa vitani, bali ni kutaka suluhu ya kweli.
Makubaliano haya yamekuja katika kipindi ambacho Marekani na Qatar zimeongeza juhudi za kuhakikisha Mashariki mwa DRC inapata utulivu wa kudumu, hasa kutokana na umuhimu wa eneo hilo kiuchumi na kimkakati.
Marekani imesisitiza amani katika ukanda huo kwa usalama wa biashara ya madini muhimu kama cobalt, dhahabu na tantalum ambazo zinahitajika sana katika teknolojia ya kisasa duniani.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayosalia ni utekelezaji wa makubaliano hayo. Historia ya DRC imejaa mikataba iyosainiwa pasi na kutekelezwa kikamilifu, hivyo kuzuka kwa mapigano upya baada ya muda mfupi.
Mchakato wa Doha unaweza tu kuwa na mafanikio iwapo kutakuwa na dhamira ya kweli na usimamizi wa karibu wa jumuiya ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni saba wamekimbia makazi yao Mashariki mwa Congo kutokana na mapigano yaliyodumu kwa miaka mingi.
Mashirika ya kiraia yameonya kuwa makubaliano yoyote hayawezi kufanikiwa bila kuwepo kwa haki kwa waathirika wa vita, kurejesha wakimbizi makwao kwa usalama na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaona kuwa Qatar imefanikiwa kufungua ukurasa mpya wa mazungumzo, lakini bado mzigo wa utekelezaji unabaki kwa Congo yenyewe na waasi wa M23. Ikiwa hakuna dhamira ya dhati, basi Doha inaweza kuwa kama mikataba.