Dk Mwinyi: Kambi za matibabu zimeleta mchango kwenye tiba

Unguja. Rais wa Zanzibar,  Dk Hussein Mwinyi, amesema Serikali inatambua mchango wa kambi za matibabu katika kufikia dhamira yake ya kutoa huduma za afya za kibingwa kwa wagonjwa, ambao wangehitaji kusafirishwa nje ya Zanzibar kwa gharama kubwa.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Julai 21, 2025 wakati wa uzinduzi wa kambi ya matibabu ya kumbukumbu ya Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati  Ali Hassan Mwinyi huko Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akizungumzia kambi hiyo kuhusisha wataalamu wabobezi wa afya kutoka Kenya, Marekani na wataalamu wa ndani wazalendo amesema ni ushuhuda hai wa mshikamano wa kimataifa na dhamira ya dhati ya Serikali kushirikiana na wadau kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

“Ni dhahiri kuwa kambi kama hizi ni fursa kwa wataalamu wetu wa ndani kujifunza na kupata uzoefu kutoka kwa madaktari hawa wa nje, kumuenzi kwa vitendo, mzee wetu na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu,” amesema.

Ameipongeza Taasisi ya The Late Ali Hassan Mwinyi Free Medical Camp, kushirikiana na wizara kuandaa kambi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Zanzibar na kumuenzi Mzee Mwinyi.

Amewasihi wananchi kuitumia fursa hiyo vizuri kujitokeza kwa wingi kwani lengo la kuweka kambi hizo ni kutoa  huduma za upimaji wa afya zao na kupatiwa matibabu, kwa watakaobainika kuwa na maradhi.

Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema kambi hizo sio tu zimeendelea kuisaidia Serikali kupunguza mzigo wa kusafirisha wagonjwa nje ya Zanzibar, lakini pia kuwaongezea ujuzi wataalamu wa ndani.

Amesema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nane wizara imeendelea kuimarisha huduma za afya hasa kukabiliana na majanga ya maradhi yasiyoambukiza ili kupunguza au kutokomeza ulemavu na vifo vinavyotokana na maradhi hayo, ambavyo vinaweza kuepukika.

Waziri Mazrui alibainisha kuwa mikakati ya wizara ni kuendelea kuimarisha majengo na miundombinu ya hospitali,ukarabati na utanuzi wa hospitali ya Mnazimmoja, ujenzi wa hospitali mpya ya rufaa na ya kufundishia Binguni, ujenzi wa hospitali ya saratani, ujenzi wa hospitali ya maradhi ya akili Pandani Pemba na ujenzi wa hospitali maalumu ya mama na mtoto.

Ameipongeza Serikali kuimarisha sekta hiyo na kuipa kipaumbele huku akiahidi kuendelea kuisimamia ili huduma zinazotolewa ziwe za viwango vya juu ambazo ni endelevu.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Mngereza Mzee Miraji amesema bado wizara inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wataalamu bingwa na miundombinu ya kutoa matibabu kwa baadhi ya wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi yasioambukiza (NCD).

Amesema hali hiyo imesababisha wizara kuendelea kusafirisha wagonjwa nje ya Zanzibar na wanaoongoza kusafirishwa ni wa moyo, saratani na mifupa.

Amebainisha kwamba wizara inaendelea na jitihada za kutatua changamoto hiyo kwa kuendelea kusomesha wataalamu wa afya na kufanya kambi mbalimbali za matibabu ya kibingwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Amesema kambi hizo zimesaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa ambapo katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa mwaka huu, wizara, taasisi na wadau mbalimbali iliweza kuratibu na kufanikisha kambi 25 za afya zilizoendeshwa na wataalamu wa ndani na kimataifa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Saudi Arabia.

Kambi hiyo ya siku saba inatoa matibabu ya maradhi mbalimbali ikiwemo ya moyo, mifupa, ngozi, maradhi ya ndani, matatizo ya mkojo na huduma za upasuaji ambazo zitafanyika Hospitali ya Wilaya ya Pangatupu.