Familia iliyotangaza dau Sh10 milioni mtoto akutwa amefariki dunia kisimani

Tabora. Mtoto Ramin Ahmed mwenye umri wa miaka 3, aliyekuwa anaishi na wazazi wake eneo la Malabi, Kata ya Mpela mkoani Tabora, amepatikana akiwa amefariki dunia katika Kisima kilichopo nyumba waliyokuwa wakiishi.

Awali, familia ya mtoto huyo ilisambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikitangaza kumzawadia Sh10 milioni yeyote mwenye taarifa alipo mtoto wao.

Akizungumzia tukio hilo, leo Jumatatu Julai 21, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha kupatikana kwa mtoto Ramin akiwa tayari amefariki ndani ya kisima.

Amesema Julai 18, 2025 saa mbili usiku Ramin alikuwa akicheza na wenzake kwenye kokoto nje ya nyumba yao wakati mama yake akiendelea kupanga vitu walivyokuwa wanahamisha kwenda nyumba nyingine ambapo baada ya muda hakumuona mtoto wake.

“Hii familia ilikuwa kwenye harakati za kuhamisha vitu kwani walikuwa wanahama nyumba hiyo kwenda sehemu nyingine na huyu mtoto pamoja na watoto wengine walikuwa wakicheza mbele ya nyumba yao kwenye kokoto lakini baada ya muda mama alipotoka tena hakumuona mwanaye, ndio akaanza kumtafuta na kuamua pia kutoa taarifa polisi,” amesema Kamanda Abwao.

Kamanda huyo amewahimiza wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuweka visima mifuniko pia kuvijengea ili kuepusha majanga kama hayo ambayo yanagharimu uhai wa watoto na haipaswi watoto kucheza karibu na visima vya maji.

“Visima vijengewe lakini pia viwe na mifuniko ili kuwaepusha watoto na ajali za kutumbukia visimani, lakini inapotokea tukio kama hili tuangalie maeneo yote hatari, mfano huyu mtoto alionekana na jirani aliyekuwa amekwenda kuchota maji katika kisima kile ndio kumuona mtoto Ramin akielea kwenye maji,” amesema.

Kwa upande wake, baba mzazi wa mtoto huyo, Sahbdad Ahmed amesema mtoto wake ameumia sehemu ya kichwa alipotumbukia katika kisima hicho ambacho ni chembamba na taarifa aliyopewa ya kiuchunguzi ni kwamba mtoto huyo alitanguliza kichwa wakati anatumbukia kisimani hivyo kujigonga kichwani.

“Taarifa ya uchunguzi wa daktari imesema mwanangu amejigonga kichwani upande wa kushoto akapasuka na jichoni pia upande wa kushoto hali hiyo ilipelekea kupoteza fahamu na kupoteza maisha.

Mi namshukuru Mungu kwa kuwa yeye ndio alimleta na yeye ndio amemchukua, naumia maskini mwanangu ameniacha lakini sina budi kusema Alhamdulilah namshukuru yeye,” ameeleza baba mzazi.