Timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, imejitoa katika mashindano maalum yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ambayo yalitarajiwa kuanza hii leo kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo Karatu yakihususha timu nne.
Taarifa hiyo imetolewa na Shirikisho la Kenya (KFK) iliyochapisha taarifa kwa umma kupitia ukurasa wake rasmi wa kijamii wa Instagram.
“Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) linapenda kuutaarifu umma kwamba Harambee Stars imejiondoa kwenye Mashindano ya Mataifa Nne ya CECAFA nchini Tanzania.”
“Uamuzi huu umetolewa kufuatia mapendekezo na ushauri kutoka kwa benchi la ufundi la timu hiyo likiongozwa na Kocha Mkuu, Benni McCarthy baada ya kufanyiwa tathmini ya kina juu ya mazingira yaliyokuwapo ambayo yalionekana hayafai kwa ushiriki wa timu na maandalizi ya jumla.”

New Content Item (1)
“Timu hiyo itarejea Kenya na kuendelea na maandalizi ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024, huku mkazo kamili ukielekezwa katika kuhakikisha kuwa wako tayari kwa kazi inayokuja.”
“FKF inasalia kujitolea kuipa timu ya taifa mazingira bora zaidi ya kushindana na kuwakilisha nchi kwa fahari.”
Mashindano hayo yalikuwa yakihusisha timu za taifa za Tanzania ‘Taifa Stars’, Kenya ‘Harambee Stars’, Uganda ‘The Cranes’ na Senegal ‘ Simba wa Teranga’ ambayo ilichukua nafasi ya Congo Brazaville iliyoshindwa kufika kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa wa Mawasiliano wa KFK, Jeff Kinyanjui alithibitisha taarifa hizo na kuongeza kuwa, timu hiyo iliyokuwa nchini tangu juzi Jumamosi itarudi Kenya leo mchana.
“Taarifa unazoiona ni kweli, hatutashiriki mashindano hayo kutokana na sababu za kiufundi ambazo KFK zimezipokea kutoka katika benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu Benni McCarthy,” amesema Kinyanjui na kuongeza;
“Tutarejea nyumbani leo mchana na kuendelea na maandalizi ya CHAN yanayotarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti.”
Aidha Ofisa Habari wa CECAFA, Andrew Oryada naye alithibitisha kuwa CECAFA imepokea maamuzi hayo ya Kenya na kwamba mashindano hayo yataendelea kama yalivyopangwa na Taifa Stars itacheza kesho dhidi ya The Cranes mchezo wa kwanza, huku Senegal ikitarajiwa kuwasili nchini Julai 23.

New Content Item (1)
“Ni kweli Shirikisho limepokea taariza za kujiondoa kwa Kenya, lakini hakufanyi mashindano hayo kutofanyika, yataendelea kwa nchi tatu zilizosalia na Taifa Stars itacheza mchezo wa kwanza kesho dhidi ya The Cranes’ na mashindano yatamalizika tarehe 27 kama ilivyopangwa awali.”
Mashindano hayo maalum ya CECAFA yalikuwa na lengo la kuziandaa vyema timu za ukanda huo kujiandaa na fainali za CHAN zirakazoanza Agosti 2-30, yakiandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.