INEC yatoa maelekezo kwa waratibu, wasimamizi wa uchaguzi mkuu

Mikoani. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa maelekezo kwa waratibu na wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ikiwataka kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu ili kuepusha malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi.

Maelekezo hayo yametolewa leo, Jumatatu Julai 21, 2025, wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya mafunzo kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, maofisa wa uchaguzi na ununuzi katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Rukwa, Shinyanga, Mbeya na Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo mkoani Shinyanga, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele amewataka washiriki kuhakikisha wanashirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote za uchaguzi kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni na maelekezo ya tume.

“Pamoja na uzoefu wenu, zingatieni mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika mfumo wa uchaguzi mwaka huu. Tofauti hizi zinahitaji mtazamo mpya na utekelezaji sahihi wa majukumu yenu,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewataka washiriki hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wazingatie mabadiliko ya sheria, hasa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani namba 1 ya mwaka 2024.

“Hakikisheni siku ya uchaguzi mnaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 kamili asubuhi pamoja na kuwasiliana na tume pale ambapo mtahitaji ushauri kuhusiana na masuala ya uchaguzi” amesema Jaji Mwambegele.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa uchaguzi, Cyprian Mbugano amesema washiriki 83 wameshiriki mafunzo hayo kutoka Mkoa wa Shinyanga na Simiyu.

Mkoani Arusha, Mjumbe wa INEC, Dk Zakia Mohamed Abubakar, amewasisitiza waratibu na wasimamizi hao kuwaajiri watendaji wenye weledi katika vituo vya kupigia kura na kuvipa taarifa mapema vyama vya siasa wakati wa mchakato wa kuapisha mawakala.

“Tume inawategemea sana. Hivyo, fanyeni kazi kwa uwajibikaji mkubwa hadi mchakato huu wa uchaguzi utakapokamilika,” amesema Dk Zakia.

Amewakumbusha washiriki kutunza siri, kutokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa kipindi chote cha uchaguzi na kuhakikisha taarifa za uchaguzi zinatolewa na tume pekee au kwa kibali rasmi cha Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Jafari Makupula, mafunzo hayo yameshirikisha washiriki 86 kutoka mikoa ya Arusha na Manyara ili kuwaandaa kutekeleza ipasavyo jukumu la kusimamia uchaguzi.

Akizungumza jijini Mwanza, Jaji wa Mahakama Kuu na Mjumbe wa INEC, Asina Omari amesema mafunzo hayo yatasaidia washiriki kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya kikatiba na kisheria.

“Mnachobeba ni dhamana kubwa. Kusimamia uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani si kazi nyepesi. Fanyeni kazi kwa uadilifu na uaminifu,” amesema Jaji Asina.

Amesema kuwa, mada 12 zitatolewa katika mafunzo, zikiwapa fursa washiriki kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu bora za kukabiliana na changamoto za uchaguzi.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Hidaya Gwando, amesema mafunzo hayo yanahusu sheria, kanuni, miongozo na mchakato mzima wa uchaguzi na yanahusisha waratibu wa mikoa, waratibu wa magereza Tanzania Bara na vyuo vya mafunzo Zanzibar.

Kwa upande wa Mwanza na Mara, jumla ya washiriki 110 wamehudhuria, wakiwamo waratibu wa uchaguzi, wasimamizi na wasaidizi ngazi ya jimbo pamoja na maofisa wa ununuzi.

Mkoani Mbeya, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Kisheria INEC, Mtibora Seleman amekemea matumizi ya lugha chafu na ukiritimba akisisitiza kwamba, mawakala wote wa vyama washirikishwe kikamilifu kulingana na sheria na kanuni zilizowekwa.

“Changamoto yoyote itakapotokea, wasiliana na Tume badala ya kusubiri mwangalizi wa uchaguzi aje kukuelekeza. Pia, zingatieni wajibu wa viongozi wa Serikali katika maeneo yenu,” amesema Seleman.

Hassan Mwandorm, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini INEC, amesema mikoa ya Mbeya na Songwe imeshirikisha wasimamizi 83 huku watatu wakitokea Mkoa wa Njombe.

Katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Mjumbe wa INEC Balozi Omar Mapuri amewakumbusha wasimamizi kuwa wanawajibika kwa Tume pekee, si mamlaka nyingine yoyote.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 20 cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, mtumishi wa Tume atawajibika kwa Tume pekee. Simamieni viapo vyenu, msikubali kuingiliwa na mamlaka zisizohusika,” ameeleza Balozi Mapuri.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Giveness Aswile amesema mafunzo hayo ni jukwaa la kubadilishana uzoefu na kukumbushana taratibu muhimu kwa kuwa, kila uchaguzi una changamoto zake.

Mkoani Rukwa, Mjumbe wa Tume hiyo, Magdalena Rwebangira amewataka wasimamizi wa uchaguzi kuepuka vitendo vya rushwa na malalamiko ambayo yanakiuka maadili ya uchaguzi, huku akisisitiza ushirikiano sawa kwa vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa.

“Nawasisitiza kuepuka rushwa na malalamiko ya aina yoyote ambayo yako kinyume na maadili ya tume katika kipindi chote cha uchaguzi,” amesema.

Agatha Kamwela, mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi wanaoshiriki mafunzo hayo, amesema amedhamiria kuyazingatia mafunzo kwa kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na miongozo ya tume.

Mkazi wa jijini Mbeya, Joyce Mussa, ameishauri INEC kutoa mwongozo wa uchaguzi mapema ili vyama vya siasa viweze kujiandaa kwa ufanisi, vikiwemo kupata ratiba na idadi ya vituo.

Naye, Daniel Rafael msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Nsimbo, mkoani Katavi, amesema ataweka kipaumbele maelekezo ya tume hiyo ili kuepuka malalamiko wakati wa uchaguzi.

Katika mafunzo hayo yaliyohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Katavi, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Manyara, Mara, Mbeya, Mwanza, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Simiyu, Songwe na Arusha, waratibu na wasimamizi walikula kiapo cha kutunza siri na kufuata miongozo iliyowekwa pamoja na sheria na taratibu.

Imeandikwa na Saada Amir (Mwanza), Peter Elias (Dar), Janeth Mushi (Arusha), Hellen Mdinda (Shinyanga), Neema Mtuka (Rukwa) na Hawa Mathias (Mbeya).