Dar es Salaam. Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikitoa kibali cha kutoa elimu ya mpigakura wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, wadau wa uchaguzi wameshauri taasisi na asasi zote za kiraia zilizoomba kufanya kazi hiyo zipewe nafasi, kwani zinatumia rasilimali zao.
INEC imetoa kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 164 kutoa elimu ya mpigakura. Pia, imetoa kibali cha uangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa.
Miongoni mwa taasisi za kimataifa zilizopewa kibali cha uangalizi wa uchaguzi mkuu ni pamoja na balozi 10 zinazowakilisha nchi zao hapa nchini. Balozi hizo ni Denmark, Netherlands, Canada, Ireland, Ujerumani, Norway, Ubelgiji, Sweden, Uingereza na Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tume, vibali hivyo vimetolewa kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 10(1)(i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 85(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 na Kanuni ya 13(1) na (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba tume, katika kikao chake maalumu kilichofanyika Julai 18, 2025, imeridhia na kutoa kibali cha uangalizi wa uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa.
“Katika kikao hicho, tume imeridhia na kutoa kibali cha kutoa elimu ya mpigakura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi za kiraia 164,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima.
Kwa upande wa taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi, INEC imezitaka ziwasilishe kwa njia ya mfumo wa usajili majina ya waangalizi na maeneo waliyopangiwa kufanya uangalizi huo kwa ajili ya kuwaandalia vibali.
Tume imeeleza kwamba katika kikao hicho imeridhia na kutoa vibali vya uangalizi wa uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa. Orodha ya taasisi na asasi husika inapatikana kupitia tovuti ya tume.
“Taasisi na asasi za kiraia zilizoridhiwa na kupewa kibali cha kutoa elimu ya mpigakura zitajulishwa kwa njia ya barua pepe kupitia mfumo wa usajili ili kujaza taarifa za kuwawezesha kukamilisha taratibu nyingine, ikiwemo kuweka orodha ya watu watakaotoa elimu hiyo,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi, ziwasilishe kwa njia ya mfumo wa usajili majina ya waangalizi na maeneo waliyopangiwa kufanya uangalizi huo kwa ajili ya kuwaandalia vibali.
Akizungumzia uteuzi wa taasisi na asasi hizo, Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe amesema ipo nafasi ya taasisi hizo kutoa elimu na kusimamia uchaguzi, hata hivyo, amehoji utaratibu uliotumika kuzipata taasisi husika.
Amesema kila taasisi iliyoomba kushiriki ilipaswa kupewa nafasi hiyo, kwani zinatumia fedha zao zenyewe na siyo za Serikali.
“Huu ni mchakato wa kawaida, na elimu inahitajika sasa kuliko miaka yote kwa sababu tuna sheria mpya na kanuni mpya. Pia tuna mgawanyiko wa watu, wengine wanasema ‘No reforms, No Election’ na wengine ‘Oktoba Tunatiki’. Ilipaswa kila aliyeomba kutoa elimu apate nafasi hiyo,” amesema.
Kwa upande wake, Mtetezi wa Haki za Binadamu, Hellen Kijo-Bisimba amesema taasisi zilizopata nafasi hiyo zinapaswa kuwa na uwezo wa kifedha na watu wenye taaluma.
“Wakati tunafanya kazi kama hiyo, nakumbuka tulikuwa na uwezo wa kutafuta watu wa kujitolea kutoa elimu. Kuna ugumu nauona katika utoaji wa elimu, upo mgawanyo wa wananchi wanaoamini uchaguzi upo na wengine wasioamini kama upo.
“Kutokana na mgawanyiko huo, unaweza kuita watu uwape elimu usiwapate. Hii ni changamoto ninayoiona,” amesema.
Mbali na hilo, Kijo-Bisimba amesema kuna mashaka mashirika ya nje kutotoa fedha kwa ajili ya uchaguzi, jambo linaloweza kuibua changamoto nyingine, akisisitiza uchaguzi huu unahitaji fedha na uwezo wa watu.
Aliyekuwa mwangalizi wa uchaguzi, Deus Kibamba amesema katika orodha ile, ameipitia na kubaini taasisi nyingi zenye uwezo wa kutoa elimu hazijapewa nafasi.
“Taasisi ninazojua zina uwezo ambazo zimepewa nafasi hazizidi nne, labda hizo taasisi ambazo zimepata vibali na hazina majina, tume inazijua.
“Taasisi nyingi sijawahi kuzisikia, na ndiyo zimepata vibali na vitaanza kutumia vibali kutafuta fedha. Kama zitakosa, basi zitabandika ofisini vibali vyao,” amesema.
Amesema miaka ya nyuma hakukuwa na utaratibu wa asasi kuomba kutoa elimu kwa mpigakura, bali tume ilikuwa inawajibika kuziita asasi zote na kuongozwa kuandaa mwongozo wa elimu kwa mpigakura ambao kila taasisi ilipewa nafasi ya kutoa elimu.
Ndani ya Tume, Kibamba amesema kulikuwa na Idara ya Ufuatiliaji Elimu kwa Umma, na ndiyo ilikuwa inaangalia usahihi wa elimu inayotolewa na kurekebisha dosari zinazobainika.
Kibamba amesema utaratibu wa kuomba vibali umesababisha taasisi nyingi zenye uwezo kukosa nafasi, huku akisisitiza kuwa hata baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vikipewa nafasi ya kutoa elimu za mpigakura.