UONGOZI wa Singida Black Stars, umemwongezea nguvu nahodha wa klabu hiyo, Kennedy Juma baada ya kuwa kwenye hatua ya mwisho kukamilisha usajili wa Vedastus Msinde.
Msinde alikuwa beki wa kati wa TMA inayoshiriki Championship na sasa ameitwa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kinachojiandaa na michuano ya CHAN mwaka huu.
Chanzo cha kuaminika kutoka Singida Black Stars kililiambia Mwanaspoti mazungumzo ya pande zote mbili yanaendelea na yapo kwenye hatua nzuri.
“Mchakato bado haujakamilika lakini mazungumzo ya pande zote mbili yapo kwenye hatua nzuri muda wowote mchezaji huyo anaweza kukamilisha usajili.”
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta beki huyo ambaye alisema ni kweli kuna mazungumzo lakini bado hajasaini mkataba na timu hiyo.
“Sijasaini mkataba, hadi sasa mimi ni mchezaji huru kwani nimemaliza mkataba wangu na TMA tukimalizana kila mmoja atafahamishwa na klabu ambayo ndio inahitaji huduma yangu.”