‘Kila la kheri, hatukudai’ maneno ya mwisho kwa Zimbwe Msimbazi

KITENDO kilichofanywa na aliyekuwa nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuwaaga wanachama na mashabiki wa timu hiyo aliyoitumikia kwa miaka 11 kimeibua hisia za mashabiki hao na mastaa mbalimbali waliomtakia kila la kheri.

Usiku wa kuamkia jana Tshabalala amewaaga wanasimba kuwa hatakuwa sehemu ya timu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka 11, ndipo walipoivamia akaunti yake na kumtakia kila la kheri.

Wengi walionekana kufurahia maisha ya beki huyo katika kikosi cha Simba wakimwambia,  wanamtakia kila la kheri na kwamba hawamdai.

Aliyekuwa kiungo wa Simba aliyeichezea pia Yanga, Saido Ntibazonkiza alikuwa sehemu ya wadau waliomtakia kheri beki huyo akiandika; ‘Kila la kheri captain’, huku mkali wa kibao cha Pawa, Mbosso yeye aliandika; ‘Kila La Heri Captain Hatukudai Kaka, Umetupambania sana’.

Mchambuzi wa masuala ya soka Ahmed Abdallah ameandika; ‘Ebwana eeh!… All the best baller, wakati Ofisa Habari wa KMC ameandika; ‘Hizi taarifa bongo hawajazoea kuziona wanazionaga tu Ulaya, football inauma sana, najua huu ujumbe zimbwe mwenye ameusoma huku anaumia sana.’

Msanii wa Bongo Fleva, Joseph Haule maarufu kwa jina la Profesa Jay naye aliacha ujumbe wake kumuaga nyota huyo, ambapo ameandika “Kila la kheri CAPTAIN kwa kweli umetupambania sana 🙏🙏”

Naye mtangazaji maarufu wa vipindi vya burudani nchini, Hamisi Mandi, maarufu kwa jina la B Dozen aliacha ujumbe akisema “All the Best Captain”

Tshabalala amedumu katika kikosi cha Simba kwa takribani miaka 11 tangu alipotua hapo mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.

Katika kipindi cha miaka 11 akiwa Simba, Tshabalala amekuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya kikosi hicho kwa kushinda mataji manne mfululizo ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021. Pia ameshinda makombe ya FA na Ngao ya Jamii.

Tshabalala pia amechangia Simba kufanya vizuri michuano ya CAF, huku timu hiyo ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita 2024-2025 na kupoteza mbele ya RS Berkane. Kabla ya hapo, imeishia robo fainali za CAF mara tano kuanzia 2018.