Kocha mpya Yanga aleta straika mwingine

KABLA hata hajatambulishwa wala kugusa uwanja wa mazoezi, kocha mpya wa Yanga, Romain Folz ametoa maagizo mazito ya kutaka asajiliwe straika mmoja wa mabao.

Kocha Folz ndiye anayetajwa kuwa mrithi wa Miloud Hamdi aliyetimkia Ismailia ya Misri na kilichobaki ni kutangazwa tu.

Hata hivyo, wakati anajiandaa kitangazwa ikielezwa tayari ameshasaini mkataba, kocha huyo amewaambia mabosi wa Yanga, kumleta Andy Boyeli.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga, ni kwamba Folz anayedaiwa tayari yupo nchini, ametaka aletewe straika huyo wa Shekhukhune United ya Afrika Kusini.

Boyeli, ni raia wa DR Congo ndio chaguo la kocha huyo akisema hana mashaka juu ya ubora wa mshambuliaji huyo.

Hata hivyo, mabosi wa Yanga wameshindwa kukubaliana na bei ya nyota  huyo aliyewahi kucheza Power Dynamos ya Zambia wakitaka kwanza kumpata kwa mkopo.

Boyeli sio jina geni kwa mabosi wa Yanga, kwani aliwahi kuingia katika hesabu zao mwaka 2023, alipokuja nchini akiifunga Simba katika mechi ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi iliyopigwa Oktoba pale Azam Complex, Chamazi.

Straika huyo aliwafunga Simba dakika ya 17, lakini akiangulia kuwapa ugumu mabeki wa wenyeji, japo mechi iliisha kwa sare ya bao 1-1, baada ya Wekundu kuchomoa  kupitia kwa John Bocco dakika ya 69.

Yanga italipa kiasi Cha Dola 20,000 katika mkataba huo wa mkopo, lakini kama itakubali uwezo alionao italazimika kutumia Dola 100,000.

Boyeli ni mshambuliaji anayejua kufunga, akiwa na nguvu za kupambana na mabekina umahiri wa kuutunza mpira mguuni.

Hatua hiyo inakwenda kufifisha zaidi hesabu za Yanga kumsajili mshambuliaji, Jonathan Sowah wa Singida Black Stars, aliyekuwa anapigiwa hesabu awali.