Iringa. Mchakato wa kura za maoni za kuwania nafasi za udiwani viti maalumu kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Iringa Mjini, umeacha tamu chungu kwa wagombea 15 kutoka kanda tano za Manispaa ya Iringa.
Uchaguzi huo ngazi ya wilaya uliofanyika kuanzia jana Julai 20 na kuhitimishwa leo Jumatatu, Julai 21, 2025 katika ukumbi wa Kichangani, ulitawaliwa na shamrashamra, hisia za msisimko na heshima miongoni mwa wagombea na wafuasi wao.
Baadhi ya wagombea walisherehekea ushindi wa kupitishwa huku wengine wakikubali matokeo kwa moyo wa ustahimilivu na kuonesha ukomavu wa kisiasa.
Akizungumza kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya kura hizo za maoni, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Aisha Mpuya aliwapongeza wagombea wote kwa nidhamu na utulivu waliouonesha katika mchakato huo, akisisitiza umuhimu wa mshikamano ndani ya chama.
Akitangaza matokeo hayo Mpuya amesema kwa upande wa Kanda ya Mkwawa, Martha Mfikwa ameshinda kwa kura 682, Christina Ngohani anayetetea nafasi hiyo amepata kura 211 na Asha Mbeju akiambulia kura 30.

Devota Chaula aliyekuwa anatetea pia nafasi hiyo Kanda ya Kitanzini/Miyomboni amepata kura 444, Augusta Mtemi kura 333 na Jamila Mwasposya kapata kura 145.
Katika kanda ya Mlandege, Husna Mtasiwa ameibuka na kura 467, Dora Nziku diwani aliyemaliza muda wake amepata kura 362 na Stella Sawani kaambulia kura 96.
Kanda ya Kihesa Mpuya amemtangaza Sara Ponela aliyeongoza kwa kupata kura 525 huku Adiliana Mnasi akipata kura 35 na diwani anayemaliza muda wake, Paschalina Lweve akipata kura 365.
Kanda ya Ruaha nayo imeshuhudia Siwema Ally akiibuka kidedea kwa kura 417, Habiba Uyagilo akipata kura 322 huku Hellen Machibya aliyekuwa akitetea kiti hicho akipata kura 189.
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi huo kwa Manispaa ya Iringa, Hassan Makoba ambaye ni Katibu wa CCM wilayani hapo, ametoa rai kwa wagombea kuendelea kushikamana na kufanya siasa za kistaarabu akisema huo ndiyo ukomavu wa kisiasa.
Mwenyekiti wa UWT wilayani humo, Christina Makwei amewasisitiza waliopitishwa katika mchujo huo, kwenda kuwatumikia wanawake na kusimamia masilahi yao wanapohudumu kwenye nafasi hizo.