KIUNGO Alphonce Mabula wa Shamakhi FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Azerbaijan amesema sasa anaanza kazi rasmi baada ya kupata uzoefu wa kucheza ligi hiyo, tangu alipojiunga nayo dirisha dogo la msimu uliopita na kucheza miezi sita.
Mabula ambaye alijiunga na Shamakhi akitokea FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya Serbia alikocheza kwa misimu miwili, aliliambia Mwanaspoti licha ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita, lakini ulikuwa wa kujifunza kwani alikuwa bado ni mgeni.
Aliongeza, anatamani kuisaidia timu hiyo kufanikisha malengo, pia kwake binafsi ili kuendelea kuwa bora zaidi.
“Msimu uliopita ulikuwa bora kwangu na ukizingatia ulikuwa ndiyo wa kwanza kwenye hii ligi. Nilikuwa kama mgeni lakini nimefanya vizuri. Msimu huu, kwa mtazamo wangu na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, utakuwa msimu bora zaidi kwa sababu nimeshakuwa na uzoefu wa hii ligi na nina uhakika nitafanya vizuri zaidi.”
“Tumeanza pre-season mapema, ndiyo maana timu zote za Ulaya zinaanza mapema. Bongo nimekaa mwezi kwa sababu kila mchezaji alipewa likizo ya mwezi mmoja. Sasa tumeingia kambini. Agosti 14 ligi itaanza.”
Katika mechi 17 alizocheza msimu uliopita, alifunga mabao matatu na kuisaidia Shamakhi kumaliza nafasi ya saba kati ya 10 zinazoshiriki ligi hiyo.