Madereva 11 wafungiwa leseni kwa ulevi Mwanza

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata na kuwafungia leseni za kuendesha magari madereva 11 kwa kipindi cha miezi mitatu kila mmoja, baada ya kubainika kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, kusababisha ajali na kuharibu miundombinu ya barabara.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatatu, Julai 21, 2025 jijini Mwanza, Kamanda wa Polisi jijini humo, Wilbrod Mutafungwa amesema hatua hiyo ni matokeo ya operesheni maalumu iliyoanza Julai 14, mwaka huu katika barabara zote za mkoa huo kuwakamata madereva wanaofanya matendo yanayohatarisha usalama barabarani.

Amesema operesheni hiyo imekuja baada ya kubaini kuongezeka kwa matukio ya ajali siku za hivi karibuni hususan nyakati za usiku, huku nyingi zikisababishwa na madereva wanaoendekeza pombe, kulewa na kuendesha vyombo vya moto.

“Ajali hizi zinasababishwa na baadhi ya madereva wanaoendekeza pombe na kisha kuendesha magari au pikipiki wakiwa wamelewa. Hii inasababisha vifo, kupunguza nguvu kazi, kuharibu magari na miundombinu ya barabara na kuiingiza Serikali kwenye gharama kubwa,” amesema Mutafungwa.

Amesema pamoja na hayo, uchunguzi unaendelea na ukikamilika watuhumiwa wote 11 watafikishwa mahakamani.

Amesema jeshi hilo halitavumilia vitendo vya ubabe vinavyofanywa na wamiliki na madereva wa magari kwa askari wawapo barabarani.

“Jeshi la Polisi limeimarisha doria kwenye barabara kuu kudhibiti vitendo vya ajali, uvunjifu wa sheria, na kuharibu miundombinu ya umma. Hatua kali zitachukuliwa kwa wamiliki wanaoruhusu magari mabovu yatembee barabarani na madereva wanaoendesha magari hayo,” ameonya Mutafungwa.

Watano mbaroni wizi wa samaki

Kamanda Mutafungwa pia ameeleza kuhusu operesheni iliyofanyika Julai 18, 2025 wilayani Magu kwa kushirikiana na kikosi cha doria majini ndani ya Ziwa Victoria, ambapo watu watano walikamatwa kwa tuhuma za kuiba samaki kwenye vizimba vya wafugaji na kuwauza rejareja.

Amesema katika msako huo wamekamata pia vielelezo ikiwemo samaki 89 aina ya sato, jokofu la kuhifadhia samaki hao na mtumbwi.

“Msako huu umefanyika baada ya kupata taarifa za vitendo hivi ambavyo wavuvi wanaamini ziwa ni la kwao na wenye vizimba hawastahili, ambapo watuhumiwa hawa walikuwa wakijihusisha na wizi wa samaki kwenye vizimba vya uwekezaji na kuuza kwa njia ya rejareja kwenye masoko,” amesema Mutafungwa.