Madina anoa makali kutetea taji Uganda

BAADA ya kushinda michuano mikubwa ya gofu ya wanawake Zambia na Ghana, Mtanzania Madina Iddi amenza rasmi maandalizi ya kutetea ubingwa wake wa John Walker Uganda Ladies Open kabla ya michuano kuanza mapema mwezi ujao, mjini Entebbe.

Agosti mwaka jana, Madina Iddi alishinda michuano mikubwa ya wanawake Uganda akianza na Uganda Ladies Open jijini Kampala  kabla ya kushinda ya John Walker, Entebbe siku saba baadaye.

Madina ambaye ameanza mazoezi  ya kujifua katika viwanja vya Gymkhana, Arusha alisema atatetea ubingwa wa John Walker pekee kwa sababu hatakuwa na muda wa kushiriki Uganda Ladies Open kwa sababu ya ufinyu wa ratiba.

“Sitaweza kushiriki Uganda Ladies Open,”  alisema Madina.

Hadi sasa haijajulikana kama kutakuwa na Watanzania wengine watakaoshiriki michuano ya Uganda kama mwaka jana na  saba walishiriki na wengi wao kufanya vizuri.

Mwezi huo pia aliibuka mshindi wa jumla wa michuano ya John Walker akimshinda Mtanzania mwenzake, Hawa Wanyeche kwa mikwaju miwili katika mashindano yaliyochezwa katika mashimo 54 ya viwanja vya gofu vya.

Madina aling’ara Uganda licha ya upinzani mkali kutoka kwa wenyeji Uganda, akiwemo bingwa mtetezi Martha Babirye.

Kabla ya kunyakua ubingwa wa John Walker, Madina alishinda mashindano mengine ya wazi yaliyofanyika Kampala baada ya kumshinda Mganda Peace Kabasweka kwa mikwaju mitano.