Madiwani saba ‘wapigwa chini’ kura za maoni CCM Moshi vijijini

Moshi. Wakati uchaguzi wa kura za maoni kwa nafasi ya madiwani wa viti maalumu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini ukikamilika, madiwani saba waliokuwa wakishikilia nafasi hizo katika wilaya hiyo wameshindwa kufurukuta huku sura mpya ziking’ara.

Katika uchaguzi huo ambao ulifanyika jana Jumapili Julai 20,2025 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, msimamizi mkuu alikuwa Constansia Kakwile akisaidiana na Ramadhan Mahanyu ambaye ni katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini.

Jumla ya wagombea walikuwa 32 wakiwa wamegawanyika katika tarafa nne zikiwamo Kibosho, Vunjo Magharibi, Vunjo Mashariki na Hai Mashariki.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na msimamizi mkuu wa uchaguzi, madiwani waliotetea nafasi zao ambao wameongoza na kura zao kwenye mabano ni Jenipha Chuwa (1,150) Irine Mariki (1,090) Gladness Mbwambo (1,037) na Jenipha Nyambo (732).

Sura mpya zilizoingia na kura zao kwenye mabano  ni Ester Kway (1,283) Pamela Chuwa (1,073) Sheila Mongi (1,062), Asia Primus Kimaryo (846) Athanasia Asenga (808) Dorine Mkandara (738), Messe Mndeme (635) na Kantate Mushi (589).

Madiwani walioshindwa kutetea nafasi zao ni Aurelia Mushi (600) Anna Amani  Lyimo (517),  Mwajabu Mchovu (498) Fabiola Massawe (285), Theresia Mlay (235), Christina Mchau (207) na Adelina Temba (78).

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo Mahanyu amesema wajumbe wamewapigia kura wagombea watatu kila mmoja.

 “Bado michakato inaendelea kwa sababu hii pia inakwenda kwenye vikao vya uchujaji na mwisho wa siku atakayeshinda, ushindi huo ni  wa CCM kwenye ngazi hiyo ya udiwani wa viti maalumu,” amesema Mahanyu.

Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Moshi Vijijini, Oliver Ngalawa amewashukuru wanawake wote waliojitokeza kwa wingi kuwania nafasi hizo.

“Nimefarijika kuona rika zote wakijitokeza katika uchaguzi huu na katika wale walioongoza kwa kura, wapo watu wenye ulemavu wawili, kundi la vijana watatu na watu wenye umri mkubwa kidogo. Niendelee kuhamasisha wanawake kunapotokea fursa wasisite kujitokeza, CCM hatuna ubaguzi,” amesema Ngalawa.

 Kwa upande wa Wilaya ya Mwanga, Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo, Mwadawa Maulid ambaye pia ni Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, amewataja walioongoza na idadi yao ya kura kwenye mabano kuwa ni Aisha Selemani (819), Halima Said (759), Neophista Gaspary (737), Lucy Mshana (694), Amina Iddi Selemani (675), Aina Makure (560) na Mwanaidi Msuya (522).

Kwa mujibu wa matokeo hayo diwani aliyemaliza muda wake, Anzirani Mfinanga ameshindwa kutetea nafasi hiyo baada ya kupata kura 492.