Dar es Salaam. Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kinondoni, Anna Makete, maarufu ‘Mama Makete’ amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Hindu Mandali Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi Katibu wa UWT Wilaya Kinondoni, Aziat Juma amesema kuwa taarifa za kifo chake walizipokea mchana wa leo Julai 21, 2025.
“Tumepata pigo, alikuwa kiongozi na mama kwenye malezi na alikuwa anakipenda Chama Cha Mapinduzi (CCM) na alikuwa hataki kuona mtu yeyote anakichafua chama na kufanya mambo kinyume na miiko ya chama,” amesema.
Aziat amemuelezea kiongozi huyo kuwa wakati wa uhai wake alikuwa anapenda kusimama kwenye miiko ya chama na alikuwa mama mwenye hofu ya Mungu.
“Tutamkumbuka daima kama kiongozi bora wakati wote mwenye kujua miiko ya uongozi na kuyatenda kwa vitendo na kuzingatia utu,” amesema.
Aziat amesema wakati wa uhai wake marehemu aliwahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ikiwemo mjumbe wa Kamati ya Siasa mkoa na Mwenyekiti wa UWT ngazi ya wilaya kwa vipindi vitatu tofauti.
Kada wa chama hicho, Wilaya ya Kinondoni, Amina Shaaban amesema taarifa za kifo zake wamezipokea kwa mshtuko mkubwa wakiwa kwenye shughuli ya kuhesabu kura za madiwani wa viti maalumu.
“Sijui nimzungumzie namna gani, lakini ni mtu ambaye alikuwa anatupambania ilikuwa hata ukimuendea unahitaji nafasi fulani anakupigania na inakuwa sasa ametwaliwa ..” amesema Amina