Mambo yanayoathiri afya | Mwananchi

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, baadhi ya mambo unayofanya au usiyoyafanya kila siku, yanaweza kuzuia jitihada zako za kuwa na afya bora.

Wakizungumza leo Jumatatu Julai 21, 2025 kwa nyakati tofauti wataalamu wa afya wamesema kutosamehe na kutosahau vinachangia magonjwa, changamoto za afya ya akili na matukio ya ukatili ikiwamo kuua na kujiua.

Daktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Mugisha Nkoronko amesema tabia hiyo humletea mtu msongo wa mawazo, humuondolea marafiki na kuwa na uchungu moyoni.

Amesema tabia hiyo pia husababisha mvurugiko wa homoni, kwa kutoa vichocheo hasi vinavyosababisha magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo kisukari, moyo na shinikizo la juu la damu.

“Kutosamehe na kutosahau huchangia tabia mbaya za kula, tabia bwete, tabia hatarishi kama kunywa pombe, kutokujijali kutokana na watu fulani kukukasirisha.

“Hilo husababisha mhusika kuharibu familia yake kwa kushindwa kuhudumia watoto, ndoa na kama ni mahali pa kazi itamfanya ushindwe kufanya kazi vizuri,” amesema.

Amesema kutosamehe na kutosahau ni chanzo cha wengi kuwa na hali ya kisasi kwa kufanya makosa makubwa yasiyosameheka kama kujiua au kuua.

Dk Mugisha ambaye pia ni Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) amesema tabia hiyo pia huchangia kuondoa utimamu wa mwili na akili.

“Mwingine atashindwa kufuata sheria za barabarani na kuhatarisha uhai wake na wengine, kuna rubani aliyekuwa akiendesha ndege aliamua kujiua yeye na abiria 270 waliokuwepo ndani ya ndege kwa kuendelea kushikilia vitu moyoni na kushindwa kusamehe,” amefafanua.

Mtaalamu wa saikolojia tiba na afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Isaac Lema amesema kusamehe na kusahau ni tabia ya kiutamaduni, haitibiwi hospitalini.

Amesema tabia hiyo inaweza kuwa chanya au hasi kutegemeana na namna mhusika atakavyolichakata jambo, kulifikiria, kulijadili na kulifanyia tathmini kisha kuachilia yaani kusamehe.

Amesema tabia ya kusamehe hutoa fursa ya kuimarisha afya ya akili kwa jamii husika na iwapo ikatokea mtu hatosamehe hupata athari hasi, kwa kubaki na jambo linalomuumiza, ambalo halijafikia hitimisho, kuzunguka kwenye fikra zake.

“Litaendelea kuleta athari nyingine kiafya na likitokea jambo jingine mwitikio wake huwa tofauti na aliyesamehe. Kusamehe si lazima aombwe msamaha, akihisi kukosewa asamehe hata kama hajaombwa msamaha.”

Dk Lema amesema mara nyingi tabia ya kusamehe na kusahau hutokana na wasifu wa mtu na tabia yake halisi.

“Wasifu hapa tunazungumzia huruma ni wasifu, kutenda matendo ya huruma ndiyo tabia, wasifu unaonesha mtu alivyo na tabia ya anachokifanya na vyote vina nafasi si kila tabia inamfanya mtu kuwa na wasifu, ila unaambatana na tabia,” amesema Dk Lema.

Akitaja tabia nyingine hatarishi kiafya, Dk Mugisha amesema kuchelewa kulala usiku, kunaathari kwa kuwa humfanya mtu kuwa na hali ya uchovu wa mwili, kinga yake ya mwili hupungua.

 “Kumbukumbu zinatengenezwa vizuri ukiwa umelala,”amesema Dk Mugisha.

Amesema kula chakula kizito usiku mwingi ni hatari zaidi kiafya kwa kuwa, husababisha damu kutozunguka vizuri mwilini na kwenda kwenye tumbo la chakula ili kusaidia mmeng’enyo, hivyo utahisi uchovu, hutalala vizuri na kuota ndoto mbaya.

Pia, amesema chakula kingi usiku hakiendi kutumika, bali huhifadhiwa na kuongeza uzito wa mwili, unene, mafuta kwenye tumbo na kusababisha hatari kwa kupata magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na ini.

“Ukila usiku mwingi ukaenda kulala, tumbo linaposaga chakula kinarudi kwenye koo unasikia kiungulia, chembe ya moyo na kiwango kibaya cha asidi na kukulete shida pia unajiweka hatarini kupata saratani ya koo la chakula,” amesema.

Dk Mugisha ametaja tabia ya mlo mbaya ‘junk food’ kwa wingi na kupuuza mlo kamili, huufanya mwili kupokea vyakula vyenye mafuta na sukari kwa wingi, hivyo kusababisha tatizo la unene kupita kiasi, mishipa kujaa mafuta na hatari ya kupata shinikizo la damu, saratani ya utumbo mpana na tumbo, kisukari na shida ya kupata choo.

“Kutofanya mazoezi ni tabia hatari kwa viungo vya mwili na wengi ukiwa mzee utatembelea mkongojo, utashindwa kupanda ngazi, utapinda mgongo, magonjwa ya mfumo wa akili, utimamu wa mwili kupungua na shida kwenye misuli na mishipa ya fahamu,” amesema.

Hata hivyo, ametaja tabia ya kutopenda kujifunza mambo mapya, humfanya mtu kuharibu afya yake au kutokuwa na uelewa wa masuala mengi hasa hatua za kujikinga na magonjwa.