UNAMKUMBUKA yule kocha aliyeiwezesha Tanzania kushiriki fainali za kwanza za CHAN 2009 zilizofanyikia Ivory Coast na aliyeifanya timu ya taifa, Taifa Stars kupendwa na mashabiki nchini kote kutokana na amshaamsha zake?
Basi kama hujui, kocha huyo Marcio Maximo anarejea tena nchini kwa mara ya tatu, lakini safari hii anatarajiwa kujiunga na KMC inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa kocha huyo kuja kufundisha Ligi Kuu, kwani mwaka 2014 aliajiriwa na Yanga na kukaa nayo kwa muda mfupi.
Ndio, kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars na Yanga, anajiandaa kurejea Ligi Kuu Bara kwa mara pili baada ya kudaiwa kumalizana na klabu ya KMC.
Maximo ambaye ni raia wa Brazili alikuja kufundisha mara ya kwanza nchini mwaka 2006 alipoteuliwa kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars hadi mwaka 2010 kisha baadaye Yanga ilimrejesha na kumuajiri kama kocha mkuu, japo alikaa kwa muda mfupi na kutimka zake.
Chanzo cha kuaminika kimelidokeza Mwanaspoti kwamba, Maximo atatua nchini Jumamosi ya wiki hii akiambatana na kocha wa viungo aliyetajwa kwa jina la Wilson Toledo ambaye atakuwa wanasaidiana katika kikosi hicho cha KMC.
Awali kocha huyo anayekumbukwa na wadau wa soka kwa namna alivyosaidia kuviboresha vipaji vya kina Jerry Tegete, Salum Telela Kiggi Makasy na wengine wakati anaifundisha Stars, alikuwa akitajwa kuhitajika na timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes kabla ya taarifa hii mpya kuibuka.
Chanzo cha ndani kilisema ujio wa Maximo utaongeza ushindani wa mechi za Ligi Kuu msimu ujao, hivyo wanaamini atakuwa na mchango mkubwa wa kuisaidia timu kushika nafasi za juu katika msimamo.
“Ni kocha anayeamini katika soka la vijana, tuliliona hilo akiwa na Taifa Stars, ambapo aliviibua vipaji vya wachezaji wengi,” kilisema chanzo hicho, huku Maximo mwenyewe alipotafutwa ili kuthibitisha taarifa hiyo naye alisema ni kweli anakuja.
“Ni kweli natarajia kuja Tanzania kwa ajili ya msimu ujao,” alisema kocha huyo aliyewahi kuzinoa timu mbalimbali zikiwamo timu ya taifa za Guyana, Costa Rica, timu za taifa za vijana za Brazili U17 na Qatar U20 mbali na klabu kadhaa.
Ujio wa Maximo unaongeza idadi ya makocha wa kigeni wenye majina makubwa kuja kufundisha Ligi Kuu kwa msimu ujao, kwani tayari Miguel Gamondi aliyewahi kuinoa Yanga, amerejea akitua Singida Black Stars, huku Azam ikiwa na Florent Ibenge kutoka DR Congo aliyekuwa akiinoa Al Hilal ya Sudan, huku Francis Baraza ambaye aliwahi kuifundisha Kagera Sugar akitajwa kurejea tena nchini kuinoa Pamba Jiji.