Mikopo asilimia 10 ilivyogeuka kete wagombea udiwani CCM

Mikoani. Chama cha Mapinduzi (CCM) leo Jumapili, Julai 20, 2025, kimefungua rasmi pazia la upigaji kura kwa wagombea walioomba nafasi ya udiwani viti maalumu.

Uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya uangalizi, huku taarifa zikieleza kuwa, baadhi ya wajumbe wanatumia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kama mbinu ya kuwashawishi wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT), ili kuwapigia kura.

Mbali ya mikopo ya asilimia 10, mikakati ya kudhibiti vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo nayo imeonekana kusimamiwa kwa umakini katika maeneo mbalimbali kunakofanyika uchaguzi huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakijinadi wagombea waliokuwa wakiomba kura, wameahidi kusimamia ipasavyo matumizi ya mikopo hiyo iwapo watapewa nafasi ya kuwa madiwani wa viti maalumu.

Mariam Kigoya amekiri kuwa, pamoja na dhamira njema ya mikopo hiyo, bado utekelezaji wake unakabiliwa na changamoto zinazowafanya wanawake wengi kushindwa kunufaika, ikiwamo urasimu na masharti magumu.

“Hadi sasa mikopo hii haijawasaidia wanawake kama ilivyokusudiwa. Tumejikuta tunachukua mikopo yenye masharti magumu na riba kubwa,” amejinadi mgombea huyo.

Naye Anifa Majura amesema utoaji wa mikopo hiyo bado hauendani na hali halisi ya wanawake wa kawaida, akidai baadhi yao wanalazimika kutumia gharama kubwa ili kutimiza vigezo vilivyowekwa, akidai vimejaa urasimu.

Baadhi ya wagombea walionekana kutumia mbinu za kuwaamkia wajumbe salamu ya “shikamoo” bila kujali tofauti ya umri, huku wengine wakitumia lugha za asili kama Kijita na Kikwaya ili kuwavutia wapigakura na kujenga ukaribu wa asili.

Katika wilaya hiyo, jumla ya wagombea 18 wamepitishwa na vikao vya CCM kuwania nafasi za uwakilishi wa wanawake kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu na watashindanishwa na vyama vingine.

Uchaguzi huo umeanza kufanyika leo Jumapili Julai 20, 2025 katika wilaya mbalimbali nchini ikiwa ni siku moja baada ya CCM kutangaza kusitisha utoaji majina ya mwisho ya wagombea wa nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi iliyopaswa kufanyika jana.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM Taifa, Amos Makalla amesema kusitishwa kwa muda wa utoaji wa fomu kumetokana na wingi wa waombaji.

“Tunahitaji muda zaidi ili kuwachambua kwa kina waombaji wote na kuhakikisha tunapata watu safi wanaokubalika mbele ya jamii. Hata hivyo, uchaguzi wa madiwani wa viti maalumu unaendelea kama kawaida,” alisema Makalla katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa ratiba ya CCM, uteuzi wa majina matatu kwa kila nafasi ya ubunge, udiwani na uwakilishi utafanyika Julai 28, 2025, baada ya vikao vya halmashauri vitakavyofanyika Julai 26.

Kwa upande wa mchakato wa uchaguzi wa madiwani viti maalumu wilayani Dodoma, zaidi ya wagombea 80 waliwasilisha maombi, lakini chama kimerudisha majina 24 pekee.

Kati ya hao, madiwani wasiozidi 12 watachaguliwa kutoka katika tarafa nne na majimbo mawili ya uchaguzi.

Awali, akizungumza katika ufunguzi, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Musoma Mjini, Stella Mtani aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanawachagua viongozi watakaosimama mbali na masilahi mengine kwa umma, lakini kutete masilahi ya wanawake na watoto.

“Huu ni muda wa kuchagua viongozi sahihi watakaosaidia wanawake kuepuka mikopo yenye riba kubwa na badala yake wanufaike na mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na manispaa,” amesema Mtani.

Utoaji rushwa ulivyodhibitiwa ukumbini

Katika kuhakikisha uchaguzi huo wa madiwani wa viti maalumu kupitia UWT unafanyika kwa uwazi na uadilifu, CCM imeweka mikakati ya kudhibiti vitendo vya rushwa, ikiwamo kuzuia wagombea kutoka nje ya ukumbi wa uchaguzi baada ya kuingia.

Kwa mujibu wa taarifa, leo wagombea walitakiwa kufika mapema zaidi ya wajumbe ukumbini, kwa madai wanaenda kupatiwa maelekezo muhimu.

Hata hivyo, walipofika kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) kunakofanyika vikao hivyo, walizuiwa kutoka nje kwa lengo la kuzuia kampeni chafu ikiwamo ya kushawishi wapigakura kwa njia zisizoruhusiwa, ambazo ni pamoja na rushwa.

Katika kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanabaki salama na huru dhidi ya vitendo vya rushwa, ulinzi mkali umeimarishwa ndani ya ukumbi wa uchaguzi kwa kushirikisha vyombo vya dola pamoja na maofisa wa CCM.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pia ilihusika kwa karibu, baadhi ya maofisa wake walivalia sare za CCM, hali iliyowafanya wasitambulike kirahisi isipokuwa kwa waliokuwa wakiwafahamu moja kwa moja.

Maofisa hao walionekana wakifuatilia kwa makini maeneo ya kuingilia, mabasi ya wagombea, na hata katika maeneo ya vyooni, baadhi ya wapambe walikuwa wakijaribu kuzungumza na wapigakura.

Mbinu hizo zimeelezwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo wa ndani wa chama.

Katika hali isiyo ya kawaida, wajumbe wa UWT Wilaya ya Dodoma Mjini wamelazimika kupiga kura mara mbili kwa wagombea wa Tarafa ya Kikombo baada ya kugundulika kuwa mpangilio wa majina ya wagombea kwenye karatasi za kupigia kura haukuwa sahihi.

Wagombea wa tarafa hiyo walikuwa wa kwanza kupigiwa kura katika uchaguzi huo, lakini wakati wakiendelea na upigaji kura, ilibainika kuwa majina ya wagombea kwenye karatasi ya kura hayakulingana na namba za utambulisho walizotambulishwa nazo awali.

Kufuatia hali hiyo, uamuzi ulifanyika wa kuchana karatasi zote za kura na kuanza upigaji kura upya kwa wagombea wa eneo hilo.

Hali hiyo ilisababisha manung’uniko miongoni mwa baadhi ya wajumbe, waliotilia shaka utaratibu wa uchaguzi huo na kuhoji ni kwa namna gani makosa kama hayo yametokea.

“Ni jambo la kushangaza. Tulitarajia kuwa kila kitu kingekuwa kimethibitishwa kabla ya kuanza kupiga kura. Hili linaumiza, hasa kwa wagombea ambao wakishindwa itaonekana kama wameondolewa kwa makosa ya kiufundi,” amesikika mmoja wa wajumbe akilalamika.

Baadhi ya wajumbe wameonya kuwa kasoro kama hizo zinaweza kuwavunja moyo wagombea na kuzua sintofahamu kuhusu uhalali wa mchakato mzima wa uchaguzi.

Kabla ya kazi ya upigaji kura kuanza, baadhi ya watu wasiokuwa wajumbe walibainika kutaka kuingia ukumbini kushiriki uchaguzi huo kinyume cha utaratibu na katiba, zinazoongoza mchakato huo.

Kata ambayo ilionekana kuwa na wajumbe wasiokuwa na sifa ilikuwa ni Mwigobero, ambako kabla ya upigaji wa kura ilibidi uhakiki ufanyike ndipo ikabainika kulikuwa na watu watano ambao si wajumbe halali.

Hali hiyo ilizua zogo na watu hao walitolewa nje ya geti kuu na mchakato wa uchaguzi ukaendelea.

Katika Wilaya ya Geita jumla ya wajumbe 3,000 wa UWT kutoka kata 50 za majimbo manne wameshiriki kuwachagua madiwani 20 kutoka miongoni mwa wagombea 46 watakaowakilisha wanawake kwenye mabaraza ya madiwani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Manispaa ya Geita.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Hashim Komba amesema mchakato huo unalenga kumpata mwakilishi wa wanawake serikalini na si mshindi au aliyeshindwa, akisisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kwa uwazi, uhuru na haki.

Hata hivyo, umakini mkubwa ulikuwepo kwa kila hatua ili kuhakikisha asiyehusika hapati nafasi ya kupenya na kila palipokuwa na mabadiliko, aliwajulisha wajumbe na walikubaliana kila hatua.

“Hatujaja kumtafuta mshindi kwa kuwa hakuna anayeshindwa, tunatafuta mwakilishi atakayesimamia masilahi ya wanawake kwenye vyombo vya maamuzi. Uchaguzi huu utakuwa wa haki na wazi,” amesema Komba.

Katibu wa UWT Mkoa wa Manyara, Angelina Milembe amesema uchaguzi huo unaendelea vyema katika maeneo tofauti ya halmashauri za wilaya za mkoa huo.

“Matokeo yakianza kutolewa nitakupa taarifa, ila hivi sasa uchaguzi unaendelea vyema kufanyika katika maeneo mbalimbali,” amesema Milembe.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda amewaasa wajumbe wa UWT mjini Babati, kutokubali kuhongwa.

Amesema mtu anayetumia fedha kusaka uongozi hawezi kuwaletea maendeleo wananchi.

“Mtu akitoa rushwa ili achaguliwe tambueni kuwa hapo hakuna kiongozi kwani atakuwa anategemea fedha ili achaguliwe na siyo uwezo wake wa uongozi na kuwasaidia wanaweza wenzake,” amesema Kaganda.

Katibu wa UWT Manyara, Christina Masagasi ambaye ni msimamizi wa uchaguzi katika halmashauri ya Wilaya ya Babati, amewataka wapigakura kuzingatia maadili ya CCM katika uchaguzi.

Katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Katibu Mwenezi wa CCM wa mkoa huo, Joseph Ryata amesisitiza amani na utulivu na kutaka wanachama wasikubali kugawanywa baada ya uchaguzi huo.

Ryata amesisitiza kuwepo kwa haki na uwazi kwa kila hatua kwa kuwa, ndiyo itakuwa kipimo pekee cha kupata wagombea waliokubalika na ambao hawatakuwa na matatizo hata wanapokwenda kuwanadi.

Imeandikwa na Habel Chidawali (Dom),Rehema Matowo (Gaita),Beldina Nyakeke (Musoma), Joseph Lyimo (Manyara) na Mary Sanyiwa (Mufindi).