Mradi Tanzania ya Kidijitali wafikia asilimia 90

Dar es Salaam. Utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya kidigitali unaogharimu zaidi ya Sh387.6 bilioni umefikia zaidi ya asilimia 90, huku upatikanaji wa huduma za baadhi ya taasisi mitandaoni ukitajwa kuwa moja ya faida.

Mradi huo wa miaka mitano, ambao Benki ya Dunia imetoa fedha, unatarajiwa kufikia tamati Oktoba 2026, ukiwa unasimamiwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Ukiwa unajumuisha vitu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya mtandao, kurahisisha huduma za umma kupitia mifumo ya kidijitali, kwa Serikali unalenga kumwezesha mwananchi kupata huduma wakati wowote na mahali popote ili kufikia malengo ya uchumi wa kidijitali.

Akizungumza katika mkutano wa wadau mbalimbali wanaohusika katika utekelezaji wa mradi huo leo, Jumatatu, Julai 21, 2025 jijini Dar es Salaam, Mohammed Abdulla Mashaka ambaye ni Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo ya Tehama nchini na Msimamizi wa mradi amesema hadi sasa mifumo zaidi ya 898 inasomana.

Tangu mradi huo ulipoanza kutekelezwa, hadi sasa mambo mbalimbali yamefanyika ili kuhakikisha unakuwa na tija stahiki ikiwemo uzinduzi wa mkakati wa uchumi wa kidijitali.

“Moja ya eneo ambalo limefanyiwa kazi ni kuhakikisha mifumo inazungumza, na hadi sasa 898 inasomana ndani ya Serikali na sekta binafsi. Hii inaifanya Tanzania kuwa kwenye ushindani wa kimataifa katika masuala ya kidijitali,” amesema.

Amesema mradi huo umekuwa ni alama ndani na nje ya nchi, kwani unaharakisha matumizi ya Tehama huku kipaumbele kikiwa ni wananchi kwa kuangalia huduma gani zinaanza kutumika.

“Hiyo ni kwa sababu tulikuwa tunaangalia kuwa ili kuboresha huduma lazima tuwe na mifumo ya msingi iweze kutekelezwa, na hili limeonekana, wananchi sasa hawana ulazima wa kwenda kufuata baadhi ya huduma katika taasisi za Serikali, badala yake wanapata huduma katika simu,” amesema.            

Ili kufikia wananchi wote, ikiwemo wa vijijini, minara 758 inayojengwa imefikia asilimia 90, huku ikiwa imeongezewa uwezo ili watu watumie huduma za intaneti itakayowasaidia kufanya shughuli zao, ikiwemo uuzaji wa mazao.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia na kiongozi wa timu ya wataalamu katika mradi huo, Paul Seaden amesema wanapoelekea mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa mradi huo, wataelekeza nguvu kwenye kukamilisha maeneo yote ya kazi yaliyosalia.

“Sasa tunatazamia kupitia kwa kina maeneo yote ya kazi yaliyosalia katika mradi huu na kusaidia kuondoa changamoto au matatizo yoyote yaliyobaki kwa nia ya kuhakikisha utekelezaji kamili wa mradi huu ndani ya mwaka mmoja ujao au zaidi kidogo,” amesema Seaden.

Seaden amesema ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unakuwa na matokeo chanya, tayari wametoa mafunzo kwa zaidi ya watumishi wa Serikali 500 kupitia kozi fupi na ndefu chini ya kipengele cha ujuzi wa kidijitali, jambo ambalo limekuwa na faida.

“Kwa sababu si tu kwa idadi ya watumishi waliopata mafunzo moja kwa moja, bali pia maarifa wanayorejea nayo kazini yanasambaa kwa timu zao kwa ujumla. Hivyo basi, 500 ni idadi kubwa kwa kipindi cha miaka miwili hadi mitatu iliyopita,” amesema.

Kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Priscus Kiwango amesema mbali na kuunganisha halmashauri, mikoa na taasisi zote zilizohamia Dodoma, pia watendaji wameanza kupimwa kidijitali.

Watendaji hao wanapimwa kupitia mfumo wa e-Utendaji na tayari taasisi 571 kutoka maeneo yaliyounganishwa zinawapima watendaji wake huko.

“Tangu kuanza kutumika kwa mifumo hii, kumekuwa na tija kwa wananchi kwani hawalazimiki kutembelea ofisi za Serikali kupata huduma, badala yake ukiwa na simu ya mkononi unaweza kujihudumia bila kujali aina ya simu unayotumia,” amesema.