Arusha. Mwili wa mtoto Karim Rahim (8), mkazi wa mtaa wa ‘Osunyai Jr’, Kata ya Sombetini jijini Arusha anayedaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya pazia, umezikwa jioni ya leo Jumatatu, Julai 21, 2025.
Mtoto Karim amefariki dunia jana Jumapili, akidaiwa kujinyonga na kamba iliyokuwa imefungwa dirishani katika moja ya chumba cha kulala.
Kwa mujibu wa wanafamilia na majirani, mtoto huyo anayeishi na bibi yake, inadaiwa alikuwa akipenda kuangalia sinema za mapigano kwenye televisheni huku akijaribisha kuyafanya baadhi ya matukio yanayoigizwa.
Asubuhi ya leo Jumatatu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alipotafutwa hakuwa na taarifa za tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.
Wakati Kamanda Masejo akisema hayo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Osunyai Jr, Silas Kimbei amesema jana mchana alipigiwa simu na majirani akiwa kanisani akielezwa kuna mtoto amejinyonga.
“Nilikuta polisi wakichukua mwili na kuondoka nao na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru na hapa kukabaki tu vilio na majonzi,” amesema.
Bibi wa marehemu, Zainab Abdallah, aliyekuwa anaishi na Karim amesema ameanza kuishi na mjukuu wake tangu akiwa mdogo na hajawahi kuwa na utundu wa aina yoyote na vitu vya hatari.
Amesema mjukuu wake aliyekuwa anasoma darasa la pili katika Shule ya Imani Academy iliyoko Sombetini, amekuwa akifanya vizuri miaka yote ya masomo yake na kushika nafasi tatu za juu.
“Jana Jumapili mimi nilitoka kidogo katika mizunguko yangu nikawaacha hapa na mama mkubwa wake ndio nikapigiwa simu Karim amekutwa na kadhia hiyo,” amesema.
Amesema kamba hiyo ambayo imefungwa katika dirisha la chumba cha kulala huwa iko hapo miaka yote kwa ajili ya kufungia dirisha baada ya kitasa kuharibika.
Mama mkubwa wa marehemu, Amina Salim amesema wakati akifanya usafi, Karimu aliingia katika chumba hicho na kuanza kucheza na wenzake waliokuwa nyuma ya nyumba kwa nje.
“Alikuwa huko chumba cha kulala akiwa amepanda juu ya kitanda akichezea, hiyo kamba ambayo miaka yote iko hapo na mimi namsikia akiita wenzake wanaocheza kwa nje kisha anajificha.”
“Ghafla nilishangaa ukimya wa muda huku wenzake wakiendelea kuita, ndio nikaingia ndani namkuta amening’inia huku akiwa amegeuka,” amesema.
Amesema baada ya kuona hali hiyo, alianza kupiga kelele na kuita majirani huku akitafuta kisu na kukata ile kamba lakini mtoto alionekana kulegea zaidi kabla ya kupewa taarifa kuwa amefariki dunia.
“Inaonekana alikuwa ameshika hiyo kamba na kujifunga akicheza na bahati mbaya ndio akateleza kutoka kwenye kingo ya kitanda alipokuwa amekanyaga na miguu kuning’inia,” amesema.
Amina amesema mtoto huyo hupenda kuangalia sinema za mapigano kwenye televisheni: “Yaani hiyo channel (anaiaja) kila mara anaangalia na anaipenda sana, hata kifurushi kikiisha leo, kesho anasumbua sana hakai hatulii hadi kilipiwe.”
Mama mzazi wa mtoto huyo, Sakina Ally (29) amesema mwanaye aliyetamani kuwa Sheikh akiwa mkubwa, alimwacha chini ya uangalizi wa mama yake baada ya kuolewa jijini Dar es salaam.
Amesema atamkumbuka mwanaye kutokana na upendo mkubwa kwa watu na zaidi kwa ndugu zake akiwemo bibi na mama yake mkubwa.
Zaidi amewataka wazazi kuwa wakaguzi wa chaneli wanazoangalia watoto wao na waangalie namna ya kudhibiti ili kuepuka majanga kama aliyokutana nayo.
“Kiukweli mwanangu alikuwa anapenda sana hizo sinema za mapigano na anaangalia huku ndani na huko nje anakocheza wanasema huwa anacheza michezo hiyo,” amesema.