Arusha. Ni simanzi na majonzi, ndivyo unavyoweza kusema ukifika katika familia ya mtoto Karim Rahim (8) mkazi wa mtaa wa Osunyai Jr uliopo kata ya Sombetini jijini Arusha anayedaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya pazia jana Julai 20,2025.
Kwa mujibu wa majirani, mtoto huyo aliyekuwa akiishi na bibi yake, alikuwa anapenda kuangalia sinema za mapigano na amekuwa akijaribu kuyafanya baadhi ya matukio yanayoigizwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema anafuatilia tukio hilo kisha atatoa taarifa.
“Ndio kwanza unaniambia ngoja nifuatilie nijue tukio na undani wake kabla ya kutoa taarifa.”
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, leo Julai 21,2025 Mwenyekiti wa mtaa wa Osunyai Jr, Silas Kimbei amesema kuwa jana mchana alipigiwa simu na majirani kuwa kuna mtoto amejinyonga, ambapo alikwenda eneo la tukio.
“Nilikuta Polisi wakichukua mwili na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru na hapa kukabaki tu vilio na majonzi” amesema.
Akizungumzia tukio hilo mkazi wa mtaa huo, Arafa Alawi amesema kuwa mtoto Karim alikuwa anaishi na bibi yake baada ya kuachwa hapo na wazazi wake wanaoishi Dar es salaam.
Alawi amesema kuwa mtoto huyo alikuwa anapenda kuangalia sinema za mapigano amekutwa na kadhia hiyo katika michezo yake anayopenda kucheza ikiwemo kuingilizia baadhi ya vitendo anavyoviona kwenye sinema za mapigano.
“Mtoto huyo alikuwa akiishi hapa vizuri tu na bibi yake na hatujaona kama alikuwa na shida yoyote na pia sidhani kama alidhamiria kufanya kitendo alichokifanya.”
Amesema, “hii itakuwa ni michezo yake anayopenda kucheza ikiwemo kuigiza sanaa za mapigano anazoona kwenye sinema, hivyo inawezekana alishika pazia akajizungusha aruke nayo kama anayopenda kufanya bahati mbaya ikamkaba.”