Bangladesh. Watu 19 wamefariki dunia nchini Bangladesh baada ya ndege ya jeshi kamandi ya anga kuanguka katika eneo la Shule na chuo cha Milestone jijini Dhaka, leo Jumatatu Julai 21, 2025.
Ndege hiyo ya mafunzo ya kijeshi kwa mujibu wa Al Jazeera imeanguka saa saba mchana wa leo wakati wanafunzi wa shule hiyo iliyopo mtaa wa Uttara, wakiwa darasani. Imeelezwa kati ya waliofariki dunia 16 ni wanafunzi, walimu wawili na rubani.
Kufuatia ajali hiyo zaidi ya watu 50, wakiwemo watoto na watu wazima, wamewahishwa hospitalini kutibiwa majeraha ya moto, kwa mujibu wa daktari wa Taasisi ya Kitaifa ya Upasuaji.
Video za tukio hilo zinazosambaa kwenye mitandao zinaonesha moto mkubwa ukiwaka karibu na bustani ya chuo hicho, huku moshi mzito ukifuka angani na umati wa watu wakiangalia kwa mbali.
Maofisa wa zimamoto wameonekana wakimwaga maji juu ya mabaki ya ndege hiyo, ambayo iligonga upande wa jengo na kusababisha uharibifu mkubwa ikiwamo kuacha tundu ukutani.
Daktari Bidhan Sarker, kutoka katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Tiba Dhaka, ameiambia Reuters kuwa:
“Mwanafunzi wa darasa la tatu alifikishwa hospitalini akiwa tayari amefariki, huku wengine watatu wa miaka 12, 14 na 40 wakilazwa kwa matibabu.”
Walioshuhudia wameeleza taharuki iliyotokea, huku video zikionesha watu wakipiga kelele na wengine wakilia wakiwa katika hali ya mshtuko.
Mwalimu mmoja wa shule hiyo, Masud Tarik, amesema:
“Nilipokuwa nikichukua wanafunzi wangu, nilisikia mlipuko kutoka nyuma… nilipogeuka, niliona moto na moshi tu.”
Kiongozi wa serikali ya mpito ya Bangladesh, Muhammad Yunus amesema uchunguzi maalumu umeanzishwa kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuhakikisha msaada wote unaohitajika unatolewa kwa waathirika.
“Hasara iliyopatikana kwa kamandi ya anga, wanafunzi, wazazi, walimu, wafanyakazi na jamii kwa ujumla haiwezi kulipika,” amesema Yunus.
Hata hivyo, Shirika la Msalaba Mwekundu la Bangladesh limeitaka jamii kutoa msaada kwa majeruhi.
Ajali hii inatokea takriban mwezi mmoja tu tangu ndege ya Air India kuanguka juu ya bweni la chuo cha udaktari huko Ahmedabad, India, na kuua watu 241 kati ya 242 waliokuwemo ndani ya ndege, pamoja na 19 waliokuwa ardhini ikielezwa kuwa ajali mbaya zaidi ya anga kwa kipindi cha muongo mmoja.