Mkurugenzi wa Watford, Gian Luca amesema kumpata nyota mwenye asili ya Kitanzania, Nestory Irankunda ni baada ya uhitaji wake kikosini hapo.
Watford inayoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza England, imekamilisha usajili wa winga huyo kutoka Bayern Munich kwa mkataba wa miaka mitano kwa ada ambayo haijawekwa wazi.
Luca alisema kocha wa kikosi hicho, Pezzolano alikuwa anahitaji huduma ya mchezaji wa pembeni mwenye kasi na nguvu kama Irankunda na wanaamini kumpata ataleta matokeo chanya kikosini hapo.
“Ni aina hasa ya mchezaji wa pembeni aliyekuwa anahitajika na Pezzolano, bado umri wake ni mdogo lakini tunamiamini kwetu atatusaidia kutokana na aina yake ya uchezaji,” alisema Luca.
Nyota huyo alionekana kuguswa kihisia baada ya kuambiwa atavaa jezi namba 66 aliyoomba apatiwe kikosini hapo na inaonekana namba hiyo ya jezi ina maana kubwa kwake.
“Unatania sio! Naweza kulia sasa hivi, Haiaminiki, nilidhani hawatanipatia, Siwezi kusubiri hii ni ya kipekee kabisa,” alisema Irankunda.
Irankunda alianza kujulikana zaidi akiwa na Adelaide United
ya Australia aliposajiliwa msimu wa 2021/22, baada ya kucheza mechi yake ya kwanza na kufunga bao la kwanza kupitia mpira wa adhabu akiwa na umri wa miaka 15.
Kijumla alicheza mechi 61 katika misimu mitatu akifunga mabao 16 na kushinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi Australia mwishoni mwa msimu 2023/24.
Msimu uliofuata akasajiliwa Bayern Munich akicheza kwa miezi sita kabla ya kutolewa kwa mkopo Grasshopper Zurich ya Uswisi.