Netanyahu hoi baada ya kula chakula chenye sumu

Tel Aviv. Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu imesema kiongozi huyo kwa sasa anapatiwa matibabu baada ya kugundulika na uvimbe wa utumbo uliotokana na kula chakula chenye sumu.

Kwa mujibu wa taarifa ya jana Jumapili Julai 20, 2025, Netanyahu alianza kujisikia mgonjwa juzi usiku ambapo alichunguzwa nyumbani kwake na Dk Alon Hershko, mkurugenzi wa idara ya matibabu ya ndani katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hadassah Ein Kerem.

Kulingana na ofisi yake, Netanyahu aliugua usiku kucha hadi pale alipogundulika kuvimba kwa utumbo.  Pia amegundulika kuwa na upungufu wa maji mwilini. Kwa mujibu wa Reuters.

Kutokana na hilo, ofisi yake imesema waziri huyo  kwa sasa atafanyia kazi nyumbani kwake kwa siku tatu zijazo. Awali, Netanyahu hakuweza kuhudhuria kikao cha baraza la mawaziri kutokana na hali hiyo.

Hata hivyo, hali yake imetangazwa kuwa nzuri baada ya kufanyiwa vipimo zaidi, inasema ofisi yake na kuongeza anapewa maji kwa njia ya mishipa (intravenous fluids) kufuatia upungufu wa maji mwilini uliotokana na ugonjwa huo.

“Kwa mujibu wa maagizo ya madaktari wake, waziri mkuu atapumzika nyumbani kwa siku tatu zijazo na atafanya mambo ya serikali kutoka hapo,” imesema ofisi yake ikinukuliwa na The Times of Israel ya nchini humo.

Netanyahu, mwenye umri wa miaka 75, amepambana na maswala ya kiafya katika miaka ya hivi karibuni, Machi 2024 alifanyiwa upasuaji wa ngiri.  Mwezi huohuo alipumzika kazini baada ya kuugua homa hiyo.

Mwaka 2023, alifanyiwa upasuaji wa kuwekewa betri ya moyo (Pacemaker). Pia, alilazwa hospitalini kwa kile alichosema wakati huo ni upungufu wa maji mwilini.  Madaktari baadaye walifichua kwamba waziri mkuu amekuwa na tatizo la moyo kwa muda mrefu.

Ripoti ya matibabu iliyotolewa Januari 2023, ilisema Netanyahu alikuwa katika hali ya kawaida kabisa ya afya, kwamba pacemaker yake ilikuwa inafanya kazi kwa usahihi na hakuna ushahidi wa ugonjwa wa moyo au hali nyingine yoyote ya matatizo.