Polisi wawili washikiliwa kwa tuhuma za mauaji Dodoma

Dodoma. Mkazi wa Kitongoji cha Mgomwa, Kata ya Matumbulu jijini Dodoma, Frank Sanga (32), amefariki dunia akidaiwa kupigwa risasi na askari polisi waliokuwa doria, alipokuwa akimsaidia ndugu yake aliyekamatwa na askari hao kwa makosa ya usalama barabarani, asipelekwe kituoni.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Julai 19, 2025, saa 7:30 mchana, maeneo ya Matumbulu jijini Dodoma, ambapo inadaiwa Frank alifyatuliwa risasi na kujeruhiwa kwenye paja, ugoko karibu na kisigino kwenye mguu wa kushoto, kabla ya kufariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi leo Julai 21, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Jeshi la Polisi linawashikilia askari wake wawili (hakuwataja majina) kutokana na tukio hilo.

Kamanda Hyera amesema siku ya tukio, askari hao walimkamata mwendesha pikipiki (jina limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi) kwa makosa ya usalama barabarani, ikiwemo kutokuwa na leseni, kutokuvaa kofia ngumu, na kuendesha pikipiki mbovu. Baada ya kukamatwa, aliwapigia ndugu zake simu ambao walifika na kutaka kuichukua pikipiki hiyo kwa nguvu, ili ndugu yao asifikishwe kituoni.

Kamanda amesema watu hao walifika kwa wingi wakiwa kwenye pikipiki tano, ambazo kila moja ilikuwa imebeba watu zaidi ya wawili na kuanza kulazimisha kuichukua pikipiki, na ndugu yao aachiwe huru.

“Katika vurugu hizo, iliwalazimu askari hao wajihami kwa kufyatua risasi kwa sababu ilionekana walikuwa wamejipanga kupambana na askari, hivyo kumjeruhi Frank Sanga kwenye paja la mguu wa kushoto na kwenye ugoko. Aliwahishwa hospitali kwa matibabu, lakini alifariki dunia akiwa anaendelea na matibabu,” amesema Kamanda Hyera.

Amesema uchunguzi wa tukio hilo ulianza mara moja, ikiwa ni pamoja na kupata maelezo kutoka kwa watu waliokuwa eneo la tukio, na hatua zinachukuliwa kwa mujibu wa ushahidi utakavyokusanywa na kwa kuzingatia sheria za nchi zinavyoelekeza.

Ametoa angalizo kwa wananchi kuwa askari polisi, kwa mujibu wa sheria, wanabeba silaha katika jitihada za kuihakikishia jamii amani, utulivu na usalama.

“Kwa hiyo, nitoe tahadhari kwa wananchi mkoani Dodoma kuacha kuwavamia na kuwashambulia askari wanapokuwa kazini, wakiwa kwenye sare na hata ambao ni askari kanzu, lakini wana vitambulisho vyao, na hasa wakiwa na silaha ili kuepusha madhara kama hayo yaliyotokea,” amesema.

Kamanda Hyera amesema si kweli kuwa Frank alipigwa risasi wakati anachunga ng’ombe, bali alikuja na kundi la ndugu waliopigiwa simu na ndugu yao, na ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kutaka kuwashambulia askari kwa kutumia fimbo aliyokuwa nayo.

Mbalina kinachoelezwa na polisi, mdogo wa Frank, David Sanga, amesema kuwa baada ya kupigiwa na ndugu yao ambaye alikuwa amekamatwa na askari hao wa doria kwa kosa la kubeba mkaa, walilazimika kwenda ili kumwekea dhamana.

Amedai walipofika eneo la tukio, ndugu yao aliwaeleza askari hao wanataka awape Sh100,000 ili wamwachie, ilihali alikuwa na kibali cha maliasili cha kusafirisha mkaa huo.

Amesema wakati wanaendelea na mabishano ya kuwataka askari hao wamwachie ndugu yao, Frank aliyekuwa ameshika fimbo ya kuchungia ng’ombe alipita katikati yao ili aende akachukue mkokoteni.

Amesema wakati anapita, askari polisi alirudi nyuma na alijikwaa, akaanguka, hivyo alipomwona Frank ameshika fimbo alidhani kuwa anakwenda kumshambulia, hivyo alifyatua risasi tatu, ambapo moja ilikwenda hewani, na nyingine mbili zilimpata kwenye mguu wa kushoto.

“Baada ya hapo walituzuia kumsogelea marehemu, na walisema yeyote atakayesogea atapigwa risasi. Ilitulazimu kutulia kwa takriban nusu saa, ndipo walipopanda pikipiki yao na kuondoka, na sisi tukamchukua kaka na kumkimbiza hospitali, lakini baadaye tukapewa taarifa kuwa ameshafariki,” amedai Sanga.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mgomwa, Noah Zakayo, amesema kuwa walipata taarifa kuwa Frank amepigwa risasi na polisi na amewahishwa hospitali, ambapo alipofika, daktari alimweleza kuwa majeraha hayo kweli ni ya risasi, na baada ya muda wakapewa taarifa kuwa ameshafariki dunia.

Mama mzazi wa marehemu (hakutaja jina), amesema alikuwa nyumbani saa saba mchana, akapigiwa simu kuwa Frank amepigwa risasi na polisi na yupo hospitali kwa ajili ya matibabu.

“Baada ya muda wakanipigia tena simu na kuniambia mwanangu Frank amefariki dunia. Ndiye alikuwa tegemeo langu, maana baba yake ni mzee na ni mgonjwa.

“Mimi mwenyewe ni mlemavu, ameniachia watoto wanne, nitawapeleka wapi mimi? Naomba Serikali inisaidie kuwatunza hawa watoto,” amesema mamam huyo huku akilia.