RC CHALAMILA AELEKEZA KUUNDWA KAMATI MAALUM KUTATUA MGOGORO WA ARDHI SAHARA-MABIBO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila ameelekeza kuudwa kwa kamati maalum itakayofanyakazi kwa muda wa siku tatu kuanzia julai 21 hadi 23 kushughulikia mgogoro umiliki wa uwanja wa Sahara kati ya wananchi wa mtaa wa mabibo na Saccos ya wafanyakazi wa shirika la posta na simu ambapo pande zote zinadai kuwa ni wamiliki halali

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sahara uliopo Mabibo Wilaya ya Ubungo RC Chalamila amesema lengo la kamati hiyo ni kijiridhisha uhalali wa vielelezo na maelezo yaliyotolewa na pande zote mbili kabla ya kutoa uamuzi hivyo anahitaji kamati hiyo kujumuisha wananchi,wanaushirika wa Sacoss ya shirika la posta na simu pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo

Aidha RC Chalamila amehimiza wananchi kuwa na utamaduni wa kuwa na nyaraka za umiliki wa ardhi yaani hati badala ya maelezo ya mdomo kwani kukosekana kwa nyaraka kunaweza kupelekea mtu kupoteza haki yake.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila ametumia mkutano huo wa hadhara kuwataka wananchi kuendelea kudumisha amani utulivu na mshikamano wa nchi wakati taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu licha ya tofauti za kisiasa kwani amani ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na makuzi ya shughuli za kiuchumi

Awali kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Wakili Albert Msando ametoa taarifa ya mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 tokea mwaka 1994 ambapo amesema kwa mujibu wa nyaraka zilizopo zinaonesha eneo hilo linamilikiwa na Sacoss ya wafanyakazi ya shirika la posta na simu.

Vilevile Kabla ya uamuzi huo wa kuunda kamati Mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila amepata nafasi ya kusikiliza maelezo ya pande hizo mbili za mgogoro ambapo wananchi wamedai eneo hilo ni kwa ajili ya michezo na wanahitaji litumike pia kujenga kituo cha afya huku mwakilishi wa saccos ya wafanyakazi wa shirika la posta na simu akieleza kuwa eneo hilo walilipata kutoka kwa iliyokuwa Sacoss ya Akilimali