Tanzania yataka juhudi za kidiplomasia kumaliza ghasia DRC

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema baada ya juhudi za kijeshi za muda mrefu kutuliza ghasia Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), kwa sasa kunahitajika hatua za kisiasa na kidiplomasia kupata muarobaini wa tatizo.

Tanzania imesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda katika kulinda amani, usalama na utawala bora ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Hata hivyo, duru za habari za kimataifa zinaeleza, DRC na kundi la waasi la M23 wamefikia makubaliano ya awali ya amani yaliyotiwa saini katika Mji wa Doha, Qatar mwishoni mwa wiki.

Azimio hilo, linalojulikana kama Declaration of Principles, linabeba matumaini mapya ya kufungua ukurasa wa mazungumzo ya kisiasa baina ya pande hizo mbili zilizokuwa kwenye vita vya muda mrefu hasa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Serikali ya Qatar kwa kushirikiana na Marekani na Umoja wa Afrika (AU), yanahusisha kusitisha mapigano mara moja, kufungua njia ya mazungumzo ya kina na kuweka msingi wa kufikia makubaliano ya kudumu kabla ya Agosti 18, mwaka huu.

Azimio hilo la kanuni, limeweka misingi mitatu ya utekelezwaji wake likisisitiza kukoma mara moja kwa mapigano yaliyodumu mashariki mwa nchi hiyo, kushushwa kwa silaha zote ifikapo Julai 29, mwaka huu na kutathmini hali ya uimarishwaji wa usalama ifikapo Agosti 18.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Julai 21, 2025 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Samwel Shelukindo, wakati akifungua Mkutano wa 27 wa Mawaziri wa SADC wa Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama (MCO).

Katika kipindi cha mwaka uliopita, amesema hali ya ukanda wa SADC umeendelea kuwa shwari, isipokuwa changamoto za usalama mashariki mwa DRC.

Ameeleza tangu 2023, SADC ilipeleka kikosi cha Samidrc kusaidia juhudi za kurejesha amani.

Hata hivyo, mashambulizi ya hivi karibuni na uamuzi wa kuondoa kikosi hicho vimeibua haja ya kuhamia njia za kisiasa na kidiplomasia.

“Ingawa kikosi cha Samidrc kilichopelekwa mwaka 2023 kimeleta mchango muhimu katika kurejesha amani, mwelekeo mpya wa kisiasa na kidiplomasia unahitajika kutatua migogoro unaoendelea baada ya kuondoka kwa kikosi hicho,” amesema.

Ametumia jukwaa hilo kupongeza hatua ya kufanyika kwa mkutano wa pamoja wa EAC na SADC uliofanyika Dar es Salaam Februari 2025, akisema ulikuwa muhimu kwa kuunganisha juhudi za Luanda na Nairobi, kwa lengo la kuratibu kwa pamoja upatikanaji wa suluhu ya kudumu.

Pia, amepongeza juhudi za Marekani na Qatar, kusaidia kuleta amani, huku msisitizo ukiwa ni kuhakikisha watu wa DRC mashariki wanapata amani ya kudumu.

“Ni lazima tuimarishe ushirikiano wa kikanda, bara na kimataifa ili tushughulikie changamoto hizi kwa haraka, kwa ufanisi na kwa gharama nafuu. Vilevile, tunapaswa kufanya tathmini ya kina ya kazi za Samidrc na Samim ili kujifunza na kuimarisha maandalizi ya operesheni zijazo,” amesema.

Katika hotuba hiyo, amesema ukanda wa SADC lazima uendelee kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa mtandao, wizi wa magari, usafirishaji haramu wa binadamu na biashara ya dawa za kulevya.

“Haya yote ni vikwazo kwa dira ya maendeleo ya SADC ya mwaka 2050. Ni wajibu wetu wa pamoja kuimarisha mifumo ya kikanda ya kuzuia na kupambana na uhalifu huo,” ameeleza.

Katika kikao hicho pia, SADC iliomboleza vifo vya viongozi wakuu wawili wa zamani wa nchi wanachama wa SADC ambao ni Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu na Makamu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, David Mabuza, sambamba na askari waliopoteza maisha kwenye operesheni ya Samidrc na watumishi wawili wa Sekretarieti ya SADC.

Tanzania kwa sasa ndiyo Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, nafasi ambayo itakabidhiwa kwa Malawi Agosti, 2025.

Kikao hicho ni maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa MCO unaotarajiwa kufanyika Julai, 24 2025.