UCHAMBUZI WA DADY IGOGO: Karata ya wagombea Viti Maalum udiwani CCM yaadhihirisha umuhimu mikopo ya asilimia 10

Nimevutiwa na habari ya Gazeti la Mwananchi la Julai 21, 2025 ukurasa wa mbele inayosema ‘Mikopo ya asilimia 10 ilivyogeuka kete ya wagombea udiwani wa CCM’, kwamba wagombea wametumia fursa za mikopo ya halmashauri kama kete kwa wajumbe ili wawapigie kura.

Ni dhahiri kuwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake amepiga hatua kubwa katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia kumi.

Katika hatua inayoonesha dhamira thabiti ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, imejiweka rekodi ya kipekee kwa kuongeza zaidi ya mara tatu ya kiwango cha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Takwimu zinaonesha mwaka 2021, wakati Rais Samia anaingia madarakani, mikopo hiyo ilikuwa ikifikia jumla ya Sh22.3 bilioni pekee.

Lakini hadi kufikia mwaka 2025, kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia Sh82.84 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh60.54 bilioni sawa na asilimia 271.

Katika mgao wa fedha hizo, vikundi vya wanawake vimepokea jumla ya Sh40.71 bilioni, vikundi vya vijana wakinufaika na Sh36.64 bilioni, huku vikundi vya watu wenye ulemavu vikipokea Sh5.48 bilioni.

Kwa mujibu wa taratibu za kisheria, mikopo hiyo inapaswa kugawiwa kwa uwiano wa asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.

Serikali imehakikisha fedha hizi zinawafikia walengwa kwa usahihi, kwa wakati na kwa uwazi.

Kupitia mikopo hii, makundi haya maalumu yameweza kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ikiwemo kilimo cha kisasa, usindikaji wa mazao ya chakula na biashara ndogondogo zinazotoa ajira kwa vijana wengine na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.

Wadau wa maendeleo na wachambuzi wa sera wamepongeza hatua hiyo wakisema ni mfano bora wa uongozi unaotanguliza maslahi ya wananchi.

Wameeleza kuwa ongezeko hilo la mikopo ni ushahidi tosha kuwa Rais Samia anatekeleza kwa vitendo ajenda ya kuwakomboa kiuchumi Watanzania wa kada zote.

Aidha, wanufaika wa mikopo hiyo wameshukuru Serikali kwa kuwawezesha kujikwamua kutoka kwenye utegemezi wa kiuchumi, huku wakieleza kuwa mikopo hiyo isiyo na riba imekuwa dira mpya ya mafanikio na matumaini kwa maisha bora.

Kwa mfano katika Mkoa wa Arusha, kwa mujibu hotuba ya taarifa ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Mkoa wa Arusha kwa miaka minne iliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi alikitaja kikundi cha vijana cha USA River kinachojihusisha na biashara ya Bodaboda kilipokea Sh100 milioni kutoka halmashauri ya Meru na kununua gari aina ya Toyota Coaster kama kikundi cha mfano kilichopiga hatua.

Serikali kupitia Wizara ya Tamisemi pia imesema itaendelea kusimamia kikamilifu utoaji wa mikopo hiyo kwa kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na urejeshaji wa fedha ili kuhakikisha mradi huu endelevu unaleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Mkoa wa Arusha umeongeza mkopo kutoka Sh3.08 bilioni (2021) hadi kufikia Sh13.55 bilioni mwaka huu. Hii ni taswira chanya ya mikoa yote Tanzania.

Kwa mafanikio haya, Serikali inaendelea kuthibitisha kuwa uwezeshaji wa wananchi si kauli ya kisiasa, bali ni hatua thabiti na madhubuti za kujenga uchumi jumuishi unaowagusa watanzania wote bila ubaguzi

Mafanikio haya ya ongezeko la mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu si jambo la kawaida, bali ni ushahidi wa wazi wa uongozi wenye dira, huruma na mtazamo wa maendeleo jumuishi.

Kwa kuongeza uwezo wa wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba, Serikali imeonesha kuwa uwezeshaji wa wananchi ni nguzo muhimu ya kujenga taifa imara, linalowajali watu wake wote.

Katika zama ambazo dunia inapambana na changamoto za kiuchumi, Tanzania imechukua mkondo wa kipekee wa kuwaamini wananchi wake na kuwawekea mazingira wezeshi ya kuibua fursa, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa.

Hatua hii ni zaidi ya takwimu; ni ushindi wa matumaini, heshima kwa utu na taswira ya serikali inayosikiliza na kutenda.

Ni wakati wa wadau wote kutoka halmashauri hadi sekta binafsi kushirikiana kuimarisha jitihada hizi ili ndoto ya Tanzania yenye uchumi shirikishi na endelevu iwe halisi kwa kila Mtanzania.

Ndiyo maana wagombea wa viti maalumu wanatumia agenda hii kama fursa.