UCHAMBUZI WA MJEMA: Tusipoamka kama taifa na kuukabili uchawa, utatupeleka kusikojulikana

Ninaona dhahiri tumeanza kuendekeza tabia ya uchawa uliopitiliza ambao kwangu nimeupa jina la ‘uchawa promax’, lakini ukweli ni kuwa una athari kubwa kwa taifa letu na polepole unaondoa uwajibikaji, maadili na uhalisia wa mambo.

Hii tabia ambayo inataka kuwa kama fani,tulizoea kuiona katika kundi dogo katika jamii yetu na ilikuwa ni aibu, sasa inavuka mipaka hadi kwa baadhi ya wasomi wakiwamo maprofesa na wenye shahada ya uzamivu (PhD) na wanazuoni.

Nasema hivyo kwa sababu huku katika jamii, machawa tuliokuwa tumewazoea ni wale ambao ‘tajiri’ akiingia baa wanamsifia na kumpamba ili atandaze pombe, lakini sasa hivi tunauona uchawa unakwenda kuua kabisa kizazi cha ukosoaji.

Kuna usemi “To lead effectively, a political leader must be open to constructive criticism and willing to learn from their mistakes”, ikimaanisha kiongozi wa kisiasa ni lazima akubali ukosoaji wenye tija na kuwa tayari kujifunza kwa makosa yao.

Ni lazima niseme na wanazuoni wengi wataungana na mimi kuwa kuna madhara makubwa sana kwa kiongozi wa kisiasa katika nchi ya kidemokrasia, kuwa machawa wanaomsifia bila kujali kama anafanya vizuri kisiasa,kijamii na kiuchumi.

Yapo madhara kama matano, moja ni kwamba timu ya wasifiaji kwa maana ya ‘chawa promax’ ambayo haiwezi kuthubutu kumkosoa au kumwajibisha mwanasiasa, inaweza kusababisha maamuzi na vitendo visivyodhibitiwa.

Lakini pili, kusifiwa mara kwa mara bila kupata mrejesho wa uwajibikaji wako kwa umma unafanya wapate uhalisia uliopotoshwa (distorted reality) juu ya utendaji wao na mtazamo wa kweli wa umma dhidi yake kwa kukubali sifa za uongo.

Tatu ni kwamba, timu ya wasifiaji au praise team inaweza kuunda chumba cha mwangwi ambapo mwanasiasa anapewa tu maoni chanya na hii inaleta hatari ya kujielekeza kufanya maamuzi mabaya kwa vile anakuwa kama vile kipofi au kiziwi.

Nne, ikiwa timu ya wasifiaji itaonekana kuwa ya uwongo au isiyokosoa ama iliyokosa maadili, inaweza kuharibu uaminifu, sifa na heshima (damage creadibility) ya mwanasiasa kwa umma na wadau kwa kuwatizama chawa wake.

Lakini tano, bila kupata mrejesho wa kweli na kwa uaminifu, mwanasiasa anaweza kukosa fursa za kujifunza kutokana na makosa, kuboresha utendaji kazi na kushughulikia masuala ya kweli yanayoitatiza jamii anayoiongoza.

Kwa nini uchawa huu ninausema una madhara makubwa ni kwa sababu ukosoaji chanya (constructive criticism) ina mchango mkubwa katika utawala wa kidemokrasia kwa sababu huchochea uwajibikaji na kuboresha maamuzi.

Ni lazima niseme hapa kupongeza au kusifia kwa jambo jema lililofanyika haijawahi kuwa ni dhambi hapa Tanzania, tatizo ni usifiaji ambao haulingani na jambo lililofanyika na wakati mwingine ni usifiaji wa kipropaganda zaidi.

Yaani hoja za msingi za wananchi au matatizo ya kweli yanayoikabili nchi na hapa simaanishi Tanzania, natoa picha ya ujumla, basi yanajibiwa kipropaganda na makundi haya ya machawa ambayo hii kazi ndio inafanya mkono uende kinywani.

Kwa hiyo ukiona katika nchi yoyote, inakabiliwa na matatizo ya msingi katika jamii halafu anatokea mtu kukuaminisha kila kitu kiko sawa huyo ni mnufaika wa mfumo au kwa maneno mengine ana maslahi na utawala uliopo madarakani.

Binafsi napenda kuwatahadharisha sana viongozi wetu wa kisiasa, wasikubali huu uchawa wetu unaoendelea hapa nchini kwani unawapofusha kuona matatizo ya kweli ya watanzania, kwa sababu machawa kukusifia uongo ndio kula yao.

Leo hii, kiwango cha chuki miongoni mwetu kinazidi kuongezeka na kimefikia katika kiwango kibaya, lakini ‘chawa promox’ hawaoni ni tatizo. Chuki zilizozalishwa na vitendo vya utekaji ni kubwa lakini Chawa Promax hawaoni.

Sasa hivi kama nilivyotangulia kusema, baadhi ya wanazuoni wakiwemo maprofesa na wenye PhD, wako radhi kufanya uchawa ili kujipendekeza kwa Rais ili wapate uteuzi (kula), kuliko kumsaidia Rais kwa kumwambia uhalisia wa jambo.

Wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, aliteua wasomi wengi kuingia katika nafasi za uteuzi, lakini baadhi walituangusha kwa sababu tuliamini wangefanya vizuri na kumsaidia Rais kuliko enzi za Nyerere tukiwa na wasomi wachache.

Ninatamani wasomi waliopo ndani ya Serikali ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan, wamweleze Rais ukweli wa hali ambayo Tanzania inapitia, na wasijibarague au kujipendekeza ili kulinda madaraka waliyopewa.

Kufanya hivyo watakuwa hawamsaidii Rais, bali wanampeleka shimoni.

Baba wa Taifa, mwalim Jullius Nyerere aliwahi kusema “Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo”, nami nasema utakuwa ni unafiki kusema hatuna tatizo la utekaji, kupotea kwa watu au kusinyaa kwa demokrasia.

Wala hatuwezi kujidanganya kuwa utawala wa sheria uko imara katika misingi yake na kwamba mihimili ya Bunge na Mahakama Iko huru, nasema hivyo kwa kuwa ukweli una sifa moja tu, kuwa ukiukataa kamwe hauwezi kugeuka kuwa uongo.

Kuna hadithi ya kifalsafa ya nguo mpya za Mfalme ambayo ni hadithi iliyoandikwa na mwandishi wa vitabu Hans Christian Andersen ambaye ni maarufu sana, iliyochapishwa mwaka wa 1837 na imetafsiriwa katika lugha zaidi ya 100.

Ni hadithi ambayo naweza kusema ina akisi hali halisi ya ‘uchawa promax’ tuliyonayo sasa na baadhi ya wanaosifiwa wanacheka hadi jino la Christmas linaonekana, bila kutafakari madhara ya uchawa niliyotangulia kuyaeleza.

Zamani za kale, kulikuwa na Mfalme alikuwa ni mpenzi na anayehusudu sana unadhifu na siku moja wajanja wa mjini, ambao nawafananisha walimwendea wakimwambia wanaweza kumshonea suti bora haijawahi kuonekana.

Wakamwambia kitambaa kitakachotumika ni maalum na kilikuwa hakionekani na wapumbavu na watu wa hali ya chini na wapumbavu, hivyo mfalme akawatuma washauri wake wawili waende kuangalia kitambaa hicho na suti ilivyoshonwa.

Lakini ukweli ni kuwa hapakuwa na kitambaa kabisa, lakini hawakuwa tayari kukiri mbele ya mfalme kwamba hawakuweza kukiona na hivyo wakakisifu kweli kweli.

Mfalme aliruhusu wajanja hao wamvike suti yake mpya maalum, iliyotengenezwa kwa kitambaa hicho maalum kisichoonekana, kwa ajili ya msafara kupitia mjini.

Ingawa mfalme alijua yu uchi, kamwe hakukubali kwa sababu alihofia kwamba labda alikuwa hafai na mpumbavu kwa kutoona kwamba alikuwa hajavaa chochote na alihofia kuwa watu wa mji wangedhani kwamba yeye ni mpumbavu.

Watu wote wa mji kwa sababu kujua mfalme anapenda kusifiwa, walimsifu sana Mfalme kwa mavazi yake mazuri, wakiogopa kukiri kwamba hawakuweza kuona mavazi hayo, mpaka mtoto mmoja mdogo aliposema:- “Lakini hana nguo”.

Wazazi wa mtoto walishangaa na kujaribu kumnyamazisha mtoto, lakini mtoto hakuwa tayari kunyamaza hata walipojaribu kumziba mdomo alifanikiwa kutamka “Mfalme yuko uchi”, baadae umma mzima wa mji ule uliungana na mtoto yule.

Simulizi hii inatufundisha kuwa watawala wanapaswa wawe makini sana na washauri wao, wapime kila wanachowashauri na wasiwakubalie kila kitu kwa sababu tu ni watu wa kumsifia kwa kila jambo analolifanya katika uongozi.

Tuchukue ushauri wa Nyerere, kwamba kila alipotaka kustaafu, baadhi ya waliokaribu yake walimshauri asisitaafu kwa kuwa bado watanzania wanamhitaji, lakini baadhi alikuja kugundua kuwa hao ni “machawa’ wanaonufaika na mfumo.

Hii nchi itaendelea kwa kuambiana ukweli, kwamba hili ni gauni na sio shati badala ya kupamba kuwa hili ni shati wakati ni gauni, tabia hii haimsaidii kiongozi wetu kufahamu mazingira halisi ya kukubalika kwa kazi zake kwa umma.

Tusipoamka na kuukabili uchawa kama taifa, utatupeleka kusikojulikana.