Dodoma. Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimesisitisha udahili wa programu tisa za shahada ya kwanza ya elimu ya ualimu katika mwaka wa masomo wa 2025/2026.
Kwa mujibu wa tangazo la chuo hicho lililowekwa mitandaoni , chuo hicho hakitopokea maombi ya udahili katika shahada za elimu ya ualimu katika sayansi, saikolojia, biashara, sanaa, sayansi ya taaluma ya habari na mawasiliano, elimu ya watu wazima na maendeleo ya jamii, malezi na unasihii, utawala na uongozi na mipango ya sera na utawala.
“Chuo kiko katika mashauriano na mamlaka husika ya udhibiti. Iwapo kutakuwa na mabadiliko au taarifa mpya kuhusiana na tangazo hili mtajulishwa mara moja,”imesema sehemu ya tangazo hilo.
Akizungumza na Mwananchi, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Lughano Kusiluka amesema wanawasiliana na wadau wote na kwamba maelezo kamili na yatatolewa baada ya mashauriano kukamilika.
“Mtu yeyote hatakiwi kupata taharuki, tunashauriana na mdhibiti, kama tunashauriana wasiwe na hofu tutawapa utaratibu tu,”amesema.
Alipoulizwa sitisho hilo limesababishwa na nini, Profesa Kusiluka amesema ni mapema mno na kutaka watu kuwa na subira watatoa maelezo.
Hata hivyo, Mwananchi linatambua kuwa usitishwaji huo ni matokeo ya mchakato unaoendelea wa mabadiliko ya mitalaa katika vyuo vya elimu ya juu nchini.
Februari 2024, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yenye dhamana ya kusimamia ubora wa elimu ya juu nchini, ilitoa mwongozo wa uandaaji na utoaji wa shahada za kada ya ualimu.
Mwongozo huo unalenga kukidhi mabadiliko makubwa yaliyofanyika kwa ngazi ya sekondari na msingi, huku ukibainisha mabadiliko makubwa ya mitalaa ya shahada za ualimu.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus amesema anachokiona kwa hatua hiyo ya kufuta kozi hizo, ni mgongano wa kisera ndani ya Serikali, kwani anasema utaratibu wa ajira unakinzana na mfumo wa programu za ualimu zinazotolewa vyuoni.
‘’Cha ajabu wadau wengi wa elimu wanaona kama ni jambo sahihi. Unajua kwa nini? Kwenye mfumo mkuu wa ajira nchini wanaosomea hizo kozi huwa hawatambuliki kama walimu. Matokeo yake wahitimu wengi wamekuwa nje kwa sababu serikali inaajiri walimu wenye masomo mawili ya kufundishia,’’ amesema.
Naye mdau wa elimu na mhadhiri wa a Chuo Kikuu cha St John cha jijini Dodoma, Dk Shadidu Ndossa amesema japo kuna mabadiliko ya mitalaa kwa sasa, kozi hizo bado zina nafasi akisisitiza kuwa UDOM ina nafasi nzuri zaidi ya kutolea maelezo hatua hiyo.
‘’Labda wanafanya mapitio ili kuziwezesha kuwa nzuri zaidi kwa sababu inavyoonekana ni kwamba wamesitisha kwa muda. Lakini kwa maana ya uhitaji kwenye soko na mtaala ulivyo, bado zinahitajika lakini kwa nini wamelitoa (tangazo) saa hizi wao (Udom) wanaweza kuwa na majibu zaidi,”amesema.
Hata hivyo, katika mtandao wa Instagram wa chuo hicho, baadhi ya wadau wa elimu walitaka uongozi utoe maelezo kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wameshaomba udahili.
“Chuo kimefanya makosa makubwa ilitakiwa tangazo litoke kabla ya wanafunzi hawajaanza kutuma maombi tangu tarehe 15. Na bado TCU guide book 2025/26 hizo kozi bado zipo kwa Udom. Why (kwa nini) hawajatoa kwenye mfumo ili zisionekane kabisa,”amehoji mtu aliyejitambulisha kwa jina la Clever _Wenger.
Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Udom, Rose Mdami amewataka wasihofie kwa kuwa watatoa utaratibu mapema na hakuna atakayekosa programu kwa uhitaji wake.