Viti maalumu udiwani, sura mpya zaibuka Moshi Mjini

Moshi. Mchakato wa kura za maoni kwa nafasi ya madiwani wa viti maalumu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Moshi umekamilika, ambapo sura mpya zimeibuka huku mmoja wa waliokuwa wakishikilia nafasi hizo akipoteza nafasi kwa kushika nafasi ya nane.

Uchaguzi huo umefanyika katika Ukumbi wa YMCA Moshi Mjini chini ya usimamizi wa Alhabibi Kibamba, akisaidiwa na Frida Kaaya, ambapo jumla ya wajumbe 688 walishiriki kupiga kura kwa wagombea 28 waliogawanyika kutoka Tarafa ya Moshi Mashariki iliyokuwa na wagombea 15 na Magharibi wagombea 13

Akisoma matokeo, Kibamba ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro, amesema katika Tarafa ya Moshi Magharibi, Pamela Shuma ameongoza kwa kupata kura 555, akifuatiwa na Theresia Mushi aliyepata kura 323. Wote wawili walikuwa madiwani wa viti maalumu kwenye baraza lililopita.

Ameeleza kuwa nafasi ya tatu imechukuliwa na Renalda Mushi aliyepata kura 299, huku Joyce Ndossi akishika nafasi ya nne kwa kura 284.

Hata hivyo, Stella Kasese, ambaye alikuwa diwani wa viti maalumu baraza lililopita, ameshindwa kutetea nafasi yake baada ya kupata kura 198, na kushika nafasi ya nane.

Kwa upande wa Moshi Mashariki, Hilda Mjema ameongoza kwa kupata kura 603, akifuatiwa na Aisha Gogo aliyepata kura 581, ambaye alikuwa akitetea nafasi yake.

Nafasi ya tatu imechukuliwa na Bius Kipingu aliyepata kura 383, akifuatiwa na Mgeni Ramadhani mwenye kura 276.