WAKATI kiungo wa Singida Black Stars raia wa Ivory Coast, Josaphat Arthur Bada akidaiwa kukaribia kujiunga na JS Kabylie ya Algeria, nyota mwingine wa timu hiyo pia, Marouf Tchakei anawindwa na Ismaily SC ya Misri ili kuichezea msimu ujao.
Taarifa ambazo Mwanaspoti lilizipata, zinaeleza Tchakei raia wa Togo ni chaguo la Kocha Mkuu, Miloud Hamdi aliyemfundisha akiwa Singida, kabla ya kujiunga na Yanga na baadaye kuondoka na kutua Ismaily ya Misri, inayotajwa kuiwinda saini yake.
Licha ya Hamdi kutoweka wazi juu ya kumhitaji kiungo huyo mshambuliaji, ila mtu wa karibu na kocha huyo alilidokeza pia Mwanaspoti, Tchakei ni mchezaji anayemvutia na yupo tayari kufanya naye kazi Misri, japo dili hilo halijafia mwishoni.
“Uongozi haujafanya uamuzi wa mwisho juu ya hatima yake kwa sababu tunaweza kuwapoteza wachezaji bora wengi wakati sisi bado hatujakamilisha baadhi ya mambo, dili lake likikamilika tutaweka wazi kwa sababu ni mapema,” kilisema chanzo hicho.
Kigogo huyo alisema tayari kuna mapendekezo ambayo kocha mpya wa timu hiyo, Miguel Gamondi ametaka yafanyiwe kazi kabla ya kuanza rasmi maandalizi ya msimu ‘Pre Season’, kwa maana ya maboresho na hadi sasa mwelekeo wake ni mzuri zaidi.
Tchakei alitua nchini kwa mara ya kwanza na kujiunga na kikosi hicho, Julai 1, 2023, akitokea AS Vita Club ya DR Congo na amewahi pia kuzichezea timu mbalimbali, zikiwemo za Gbikinti FC de Bassar na ASKO de Kara zote za huko kwao Togo.
Kwa msimu wa 2024-2025, nyota huyo alihusika na mabao 10, ya Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho cha Singida na alifunga sita tu na kuasisti manne, akikiwezesha kumaliza nafasi ya nne na pointi 57 na kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika.