‘Wakumbukeni, waombeeni dua waliotangulia mbele ya haki’

Pemba. Mwenyekiti mstaafu wa  Chama cha ADC, Hamada Rashid Mohd ametoa rai kwa  wanasiasa nchini  kuwaenzi viongozi waliotangulia mbele ya haki kwa kuendeleza  mazuri waliyoyaanzisha.

Amesema hiyo ni sehemu ya  kuwaombea dua waliotangulia kutokana na michango yao kwa Taifa na jamii badala ya kuwasifu kwa harakati za kisiasa pekee.

Hamada amesema hayo leo Jumanne Julai 21, 2025 katika Kijiji cha Mtambwe, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskadini Pemba baada ya kutembelea kaburi  na kusoma dua ya aliyekuwa makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika ziara hiyo, Hamada amepata chakula cha mchana na wanafunzi wa Al-Madrasat Sharrif iliyoanzishwa na marehemu Maalim Seif katika Kijiji cha Nyali, eneo alikozaliwa.

Amesema  viongozi kama hao wanahitaji kuombewa dua na kuendeleza mema waliyoyaacha enzi ya uhai wao.

Amesema Maalim amefanya mambo makubwa yaliyoacha alama Zanzibar sambamba na kusisitiza amani, umoja na mshikamano kwa wananchi.

“Tunawajibu sisi wanasiasa kuwaenzi viongozi waliotangulia mbele ya haki, hii ni  kutokana na mambo makubwa waliyolifanyia Taifa hili, na watu wa mwanzo kutekeleza hili ni viongozi wa kisiasa,” amesema Hamad.

Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo mstaafu amewasisitiza wanafunzi alioambatana nao kuisoma na kuifadhi Qur-an  Tukufu kwa kuwa  ndio msingi wao wa maisha ya duniani na kesho akhera.

“Vitu hivi alivoviacha Maalim ni vya kuendelezwa, alianzisha Madrasa katika uhai wake kwa lengo la vijana kupata elimu ya msingi, hivyo vitu vinahitaji kuendelezwa kwa juhudi kubwa na maarifa,” amesema Hamad.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanakijiji cha Nyali Mtambwe, Khatib Bakar Maftah amemshukuru mwenyekiti huyo mstaafu kwa kuungana na wananchi na wanafamilia ya marehemu Maalim Seif kumuombea dua.

Amemuomba awafikishie salam zao kwa viongozi wa Serikali, wakumbuke kuwajengea barabara kijijini kwao kwa sababu ni kero ya muda mrefu.

“Tunashuru kwa kuja kuungana na wananchi wa Mtambwe kumuombea dua (Maalim), tunakuomba changamoto zetu utufikishie serikalini hasa hii ya barabara yetu ya Kijiji cha Nyali Mtambwe ni mbovu, inahitaji kutengenezwe,”amesema Khatib.