Wanaohujumu miundombinu ya majitaka Dar waonywa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), imewataka wananchi kuacha kutupa taka ngumu kwenye miundombinu ya majitaka na kuwa wa kwanza kutoa taarifa kwa anayeihujumu.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Julai 21, 2025 na Mbaraka Mpala kutoka Dawasa, baada ya kushuhudia maboresho ya miundombinu ya majitaka katika mtaa wa Sinza A, jijini Dar es Salaam.

Amesema baadhi ya watu wanaohujumu miundombinu ya majitaka kwa kuiba mifuniko ya chemba za majitaka na kusababisha taka ngumu kuingia, jambo linalosababisha kuziba kwa chemba na kutiririsha majitaka hovyo mtaani.

Mpala amesema eneo hilo lilikabiliwa na changamoto katika mifumo ya majitaka hali iliyosababisha kuziba kwa chemba na kutiririsha majitaka mtaani, jambo ambalo kwa sasa wamelifanyia kazi na hali ni shwari.

Mkazi wa mtaa wa Sinza A, Haji Ally amepongeza hatua hiyo kwani utiririkaji ovyo majitaka ukikithiri huathiri afya za wakazi hususan watoto.

“Ni jambo jema kazi hii imefanyika, chemba hizi kuwa wazi ilisababisha baadhi ya wananchi kutupa taka ngumu katika mifumo hiyo na kuziba, majitaka yakitiririka mtaani afya za watu zinakua hatarini kupatwa na magonjwa ukizingatia tuna watoto wadogo hapa mtaani,” amesema Haji.

Katika hatua nyingine, wananchi wanaonufaika na mradi wa maji Pangani- Kibaha wameipongeza Serikali kwa kuwatafutia suluhisho la tatizo la ukosefu wa huduma hiyo.

Kauli za wananchi hao zimekuja baada ya kupita wiki moja tangu Dawasa kuanza kufikisha miundombinu ya ujenzi kwenye eneo la mradi ikiwemo mabomba ya kusafirisha maji ya ukubwa wa inchi 6 yatakayolazwa kwa mita 1,100.

Mradi huo ulisainiwa mwaka 2023, unatarajia kuwanufaisha zaidi ya wananchi 14,868 wa maeneo ya Kibaha- Msufini, Lulanzi, Tamcona Pangani, ukiwa na thamani ya Sh9.8 bilioni.

Utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kusafirisha maji kiasi cha lita za ujazo wa milioni 5.2 kwa siku ambayo ni mahitaji ya miaka 20 ijayo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi Mwenyekiti wa Mtaa wa Pangani, Jitihada Hussein ametoa ameishukuru  Serikali kwa kusikia kilio chao cha maji na kuwaondolea changamoto ya kuyafuata maji mbali.

Mkazi wa mtaa wa Mtakuja, Pili Maswali ametoa shukurani kwa Serikali kwa kuwakumbuka wanawake ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata maji.

“Mwanzo tulikuwa tunapata maji kupitia visima vifupi, tumefurahi mradi huu utakuwa mkombozi wa maendeleo yetu na shughuli za maendeleo zitaonekana sasa,” amesema Pili.