Mbeya. Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mbeya Mjini wamewapitisha madiwani wa viti maalumu 12 kati ya 36 waliokuwa wameomba ridhaa ya kugombea nafasi hizo, huku wakiwatema wanne waliokuwa wakitetea nafasi hizo.
Mchakato wa kupiga kura za maoni kwa chama hicho Mbeya Mjini ulianza jana Jumapili, ambapo leo Jumatatu Julai 21, 2025 umemalizika na kuwapata washindi ambao wanasubiri vikao vya juu kuamua hatima yao.
Walioondolewa kwa kura zao kutotosha ni Zabibu Kimata na Agatha Ngole waliokuwa katika Tarafa ya Sisimba, huku Mariamu Kabuje na Agnes Mangasila wa Tarafa ya Iyunga.
Waliopenya kwenye kura hizo ni Frolence Mwakanyamale aliyepata kura 907 kutoka Tarafa ya Sisimba, akiungana na Atupere Msai (851), Rose Kilemile (768), Syirichelia Kato (766) na Magdalena Komba aliyepata kura 716.
Kwa upande wa Tarafa ya Iyunga iliyohitaji washindi saba, wamepita Catherine Ipopo aliyepata kura 875, Fatuma Bora (852), Mariam Kikasi (801), Lucia Mwanasinjale (774), Furaha Ndunguru (760), Mary Mwaijumba (758) na Magreth Kalonga aliyepata kura 741.
Akizungumza kabla ya kutangazwa matokeo hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Mohamed Mavallah, amewaomba watiania kuwa watulivu, akitahadharisha kuwa waliopita si washindi moja kwa moja kwa kuwa ipo hatua nyingine itafuatiliwa zaidi.