Watatoboa? | Mwananchi

Dar es Salaam. Watatoboa? Ndilo swali linaloibuka kuwahusu makada wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Humphrey Polepole na Askofu Josephat Gwajima, iwapo watavuka vikao viwili vya kitaifa vya chama hicho bila uamuzi wowote dhidi yao.

Vikao hivyo ni Kamati Kuu (CC), inayotarajiwa kuketi Julai 26, na Halmashauri Kuu (NEC) ya dharura iliyoitishwa Julai 28, 2025.

Awali, kikao cha Kamati Kuu kilikuwa kimepangwa kufanyika Julai 19, 2025, na Halmashauri Kuu ingekutana Agosti 20, 2025 ambapo, pamoja na mambo mengine, ni kuteua majina ya wagombea ubunge na uwakilishi baada ya kura za maoni kufanyika.

Hata hivyo, kikao cha Kamati Kuu kimeahirishwa hadi Julai 26 na NEC itakutana Julai 28, 2025.

Hii ni kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, aliyesema uchujaji wa wagombea haujakamilika.

Makalla alieleza kuwa sababu za kuahirishwa kwa vikao vya uteuzi ni kutokamilika kwa mchakato wa uchujaji wa makada waliotia nia.

Kutokana na hilo, alisema hatima ya makada watakaouteuliwa kwenda kupigiwa kura kuwania udiwani, ubunge na uwakilishi kupitia CCM itajulikana Julai 28, 2025.

Hofu ya kutoboa kwao inatokana na kauli zao za siku za karibuni zinazodaiwa kupotosha msimamo na uamuzi wa Mkutano Mkuu wa chama hicho, ambao umechukuliwa na makada wenzao kama kosa la usaliti kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili ya CCM.

Hata hivyo, jitihada za kumpata Balozi Polepole ama Askofu Gwajima ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, juu ya shinikizo hilo la kutimuliwa hazikuzaa matunda kwani hawakupatikana.

Juzi, Balozi Polepole aliitisha mkutano na wanahabari kwa njia ya mtandao na kukosoa uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Januari 18–19, 2025, uliompitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kwa upande wa Askofu Gwajima, alikosoa utendaji wa Serikali kwa madai kuwa imeshindwa kudhibiti utekaji na kupotea kwa watu, huku akiitaka CCM ikubali kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi ili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiingie kwenye mchakato huo.

Swali la kuwa kama watatoboa linapata mashiko zaidi hasa baada ya kuibuka shinikizo la adhabu kutoka kwa baadhi ya makada wa chama hicho, wakitaka hatua zichukuliwe dhidi ya wawili hao kwa hoja kuwa wanatoboa mtumbwi katikati ya safari.

Historia nayo inakoleza swali hilo. Kwa vitendo vinavyofanana au kukaribiana na vya Polepole na Askofu Gwajima ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Februari 10, 2025 chama hicho kilimfuta uanachama kada wake, Godfrey Malisa, vivyo hivyo Februari 28, 2020 kilimvua uanachama Bernard Membe (sasa ni marehemu) na kumkaripia Katibu Mkuu wake mstaafu, Abdulrahman Kinana.

Mstari wa kutoboa unazidi kuwa mwembamba, hasa ukirejea kifungu cha 8(ix) cha Kanuni za Uongozi na Maadili ya CCM, kinachoyataja matendo ya Balozi Polepole na Askofu Gwajima kuwa usaliti, na kwamba hilo ndilo kosa kubwa kwa chama hicho.

Kifungu hicho (a) kinasema: “Ikithibitika kuwa mwanachama huyo anayetenda hayo kwa makusudi, basi atakuwa amefukuzwa daima.”

Ix(b) inaeleza kuwa ikiwa ametenda hilo kwa ujinga au bahati mbaya, adhabu yake ya kuangaliwa ni miezi 48, na kwamba adhabu ya kufukuzwa uanachama itatangazwa hadharani.

Katika mahojiano yake na moja ya vyombo vya habari hivi karibuni, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Fadhili Maganya aliwataka Balozi Polepole na Askofu Gwajima watoke hadharani na wenzao kueleza dhamira zao za kutaka nafasi za juu za uongozi badala ya kueleza wanayoyaeleza.

“Haya ni maigizo tu wanayoyafanya kwa Watanzania. Watu hawa ni viongozi serikalini na mwingine ni mjumbe wa mikutano kadhaa ya CCM. Wangeweza kushauri, kumtafuta Rais moja kwa moja na kumweleza mawazo yao na hatimaye tukapata suluhisho la pamoja.

“Lakini kwa vile hawana nia ya dhati, basi wameamua kufanya walichofanya kujipatia umaarufu kwa jamii. Niwaambie jamii sasa imeamka na inajua yupi yupo kwa ajili yao na yupi anasimamia maslahi binafsi,” alisema Maganya.

Alisema kama chama hakitasimama kidete dhidi ya makundi hayo, kuna hatari ya kupoteza mwelekeo wa kihistoria ambao umekifanya CCM kitawale na kufanikiwa tangu mfumo wa vyama vingi uanze.

Kada mwingine, Khamis Mgeja amesema Polepole anapaswa kuogopwa na ameisihi CCM isimlee kwa kile alichosema, anatoboa mtumbwi katikati ya safari.

“Haiwezekani mtu anatoboa boti mnasafiri naye, halafu anatoa maneno ya kinafiki kuwa ataendelea kuwa mwana CCM. Huo ni unafiki uliobobea, huyu ni mwanaharakati,” amesema Mgeja aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.

Ukiacha shinikizo hilo, habari kutoka ndani ya CCM zinadai kuwepo kwa taarifa za ama kujadiliwa au kufukuzwa kabisa kwa makada hao.

Imeelezwa muda wowote kuanzia sasa NEC itakutana, na pamoja na mambo mengine, huenda suala la makada hao likawa sehemu ya ajenda.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu na NEC aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema kilichofanywa na Polepole ni usaliti kwa kuwa amepinga uamuzi wa Mkutano Mkuu.

Amesema haiwezekani mwanachama wa CCM akaibua hoja kwamba utaratibu wa Mkutano Mkuu haukufuatwa, wakati kila kitu kimefanywa kwa mujibu wa kanuni.

“Polepole akasome Katiba kwamba Mkutano Mkuu una mamlaka ya kuelekeza kikao chochote kifanye maamuzi. Na kwa mujibu wa kanuni, Mkutano Mkuu unaweza kuitwa na Mwenyekiti au theluthi mbili ya wajumbe wa NEC,” amesema.

Mjumbe huyo amesema anachotaka kufanywa na Polepole ni kuuaminisha umma kwamba Rais Samia anamaliza kipindi cha pili mwaka huu, ilhali sivyo inavyopaswa kuwa.

“Aliyewekewa ukomo wa kuongoza kwa vipindi viwili kwa mujibu wa Katiba ni Rais, siyo Makamu wa Rais. Rais Samia alikuwa Makamu na amekuwa Rais kwa awamu moja, ana haki ya kuongoza kwa kipindi cha pili,” ameongeza.

Amesema kilichofanywa na kada huyo ni usaliti kwa kuwa amepingana na uamuzi wa kikao halali, na kwa kosa hilo, kanuni inaelekeza afutwe uanachama na itafanywa hivyo.

Ukiacha kinachoelezwa na viongozi ndani ya CCM, wachambuzi wa masuala ya siasa nao wana mtazamo huo, wakisema uwezekano wa makada hao kuchukuliwa hatua kali ni mkubwa.

“Wamekuwa wakitoa matamko ambayo ni wazi yanakwenda kinyume na msimamo rasmi wa chama. Ndani ya CCM, jambo hilo ni nadra kuvumiliwa. Inaonekana wanasema mambo ambayo chama hakitaki kuyasikia, na hayo pekee yanatosha kuwaondoa,” amesema Dk Onesmo Kyauke.

Hoja inayofanana na hiyo imetolewa pia na Profesa Makame Ali Ussi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), anayeeleza kuwa chama hicho hakina uwezekano wa kuacha matamshi ya makada hao bila kuchukua hatua, lakini hadhani kama watafutwa uanachama.

“Hata kama hawatafukuzwa, mikutano itashughulikia mwenendo wao. Wanaweza kuonywa au kupewa karipio. Ni vigumu kufikiria chama kikiendesha mikutano muhimu kama hii, halafu kisijibu lolote,” amesema.

Amekwenda mbali zaidi na kueleza, hakuna ambacho CCM itapoteza iwapo itaamua kuwaondoa makada hao, kwani ina wanachama wengi.

Kuhusu mchujo wa wagombea

Kwa upande mwingine, Julai 28, NEC itakuwa na kibarua cha kupitisha majina ya watiania watakaorudishwa kupigiwa kura za maoni, jambo lililosogezwa mbele kutoka Julai 19.

Ingawa CCM inasema imesogeza mbele kukamilisha mchujo huo, wapo wadau wa masuala ya siasa wanaohusisha uamuzi huo na hofu ya chama hicho kukataliwa na makada wake, jambo ambalo huenda likaibua kuhama kwa baadhi yao.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa amesema kwa upande mmoja kunaweza kuwepo hofu hiyo.

Lakini amesema hata kama chama kitaahirisha ratiba yake kwa hofu ya wanachama kuhama, bado hali hiyo haiwezi kuzuiwa kwa sababu ni sehemu ya mzunguko wa kisiasa na wanaofanya hivyo ni haki yao.

“Hata ukichelewesha ratiba, kama kuna watu waliokusudia kuhama, watahama tu. Hii si jambo jipya. Katika uchaguzi wa mwaka 2015, tulishuhudia mwanasiasa mkubwa akihama kutoka CCM na kujiunga na upinzani, japo athari zake hazikuwa kubwa kama zilivyotarajiwa,” amesema Dk Kahangwa.

Hata hivyo, amehusisha uamuzi wa CCM kusogeza mbele ratiba hiyo na malalamiko kutoka kwa makada wake waliokatwa majina, akisema ni muhimu chama kikatilia maanani na kuyashughulikia kikamilifu kabla ya kutangaza majina ya mwisho ya wagombea.

“Kama kuna malalamiko kuhusu mchakato, hasa ya kiufundi, ni busara chama kukaa chini kuyapitia kwa kina. Taasisi makini haitakimbilia kukamilisha mchakato kabla ya kujiridhisha kuwa kila hatua imefuatwa kwa usahihi,” alisema.