WATENDAJI UCHAGUZI WATAKIWA KUTOA TAARIFA KWA VYAMA VYA SIASA

 

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa uchaguzi mkuu kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu leo Julai 21, 2025. Mafunzo hayo yamefanyika mkoani Shinyanga.  

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa uchaguzi mkuu kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu leo Julai 21, 2025. Mafunzo hayo yamefanyika mkoani Shinyanga.

Washiriki wa mafunzo hayo ambayo yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo kutoka majimbo yote ya Mikoa ya Shinyanga na Simiyu. 

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ndg. Cyprian Mbugano akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ambapo pia alitoa mada. 

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kama hayo kwa Kisiwani Pemba, Zanzibar ambapo amewaasa watendaji hao kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndg Adam Mkina ambaye ni Mkurugenzi wa INEC ofisi ya Zanzibar akizungumza jambo. 

Washiriki wa mafunzo hayo ambayo yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo kutoka majimbo yote ya Kisiwani Pemba, Zanzibar.

*******

Na. Mwandishi wetu, Shinyanga
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka
watendaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutoa taarifa mapema kwa vyama vya
siasa kuhusu utaratibu wa kuwaapisha mawakala.
 
Hayo yamesemwa mkoani Shinyanga leo Julai 21,
2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya
Rufani, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu kwa tarehe itakayotangazwa
na Tume.
 
“Wakati wa kuapisha mawakala, toeni taarifa
mapema kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya Tume na
kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha
kupanga mawakala,” amesema Jaji Mwambegele.
 
Amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha vifaa
vya uchaguzi wanavyopokea kutoka Tume, wanavihakiki, kuvikagua na kuhakikisha
vinasambazwa kwenye vituo vyote na kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya
uchaguzi vinavyohitajika mapema.
 
Amewataka kuhakikisha kuwa siku ya uchaguzi
wanaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa
1:00 kamili asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale ambapo ushauri
utahitajika kuhusiana na masuala ya uchaguzi.
 
Akifungua mafunzo kama hayo Kisiwani Pemba,
Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa
Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk amewaasa watendaji hao kufanya kazi kwa
kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa
na yatakayotolewa na Tume.
 
 “Jitahidini
na mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa
uchaguzi. Hakikisheni mnazingatia ipasavyo Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na
maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume,” amesema Jaji
Mwambegele.
 
Amewataka kuwashirikisha wadau wa uchaguzi kwenye
maeneo wanayopaswa kushirikishwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo
na maelekezo ya Tume.
 
Amewakumbusha kuhusu wajibu wao wa kuhakikisha
wanavitambua vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo
husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi
kufanyika kwa utulivu na amani.
 
“Ajira za watendaji wa vituo zizingatie
kuajiri watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo, waadilifu na wachapakazi
na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya
shughuli za uchaguzi,” amesema Jaji Mbarouk.
 
Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tatu kwenye
mikoa mbalimbali nchini kwa siku tatu na yanawajumuisha waratibu wa uchaguzi,
wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo.


Tume imeyagawa mafunzo hayo kwenye awamu
mbili ambapo awamu hii ya pili inahusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Kusini
Pemba, Kaskazini Pemba, Mwanza, Mara, Dar es Salaam, Pwani, Rukwa, Katavi,
Manyara, Arusha, Songwe na Mbeya.
 
Awamu ya kwanza ilifanyika tarehe 15 hadi 17
na ilihusisha watendaji kutoka mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma, Kaskazini
Unguja, Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Geita, Kagera, Mtwara, Lindi, Tabora,
Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Ruvuma, Iringa na Njombe.
Hakimu mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Goodselda Kalumuna akitoa maelezo kabla ya kuwaapisha washiriki hao wa mafunzo kwa watendaji wa Uchagzi Mkuu ambapo aliwaongoza kula kiapo cha kujitoa uanachama na kutunza siri wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ya Uchaguzi. 


Washiriki wamafunzo kutoka Shinyanga na Simiyu wakila kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri. 

Washiriki wamafunzo kutoka Kisiwa cha Pemba, Zanzibar wakila kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri.