Geita. Watumishi wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoani Mwanza wamepoteza maisha baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka boda ya Mtukula iliyopo mkoani Kagera kwenda Mwanza, kuacha njia na kupinduka katika eneo la Bwawani Mji mdogo wa Katoro wilayani Geita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema imetokea usiku wa Julai 20, 2025 baada ya dereva kuzidiwa na uchovu na kushindwa kulimudu gari.
Kwa mujibu wa Kamanda Jongo gari hilo mali ya TRA likiendeshwa na Julius Dismas (31) lilikuwa likisindikiza mzigo uliokamatwa boda ya Mtukula kwenda Mwanza na lilipofika Katoro saa 10 alfajiri lilipata ajali.
“Dereva amepata majeraha ya kawaida na kuruhusiwa, lakini abiria wake ndio walipoteza maisha, hii ni ajali ya usiku inawezekana wenzake walikuwa wamelala hawakuona, huyu dereva alitoka Mwanza akaenda mpaka Mtukula na kurudi,”amesema Jongo.
Kamanda Jongo amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Maofisa wa forodha Emmanuel Leonard (33) na Mwita John (28) wote wakazi wa Mwanza.
“Uchovu ulimsababishia kushindwa kumudu gari na kutokana na hali hiyo, gari lilihama upande wake wa barabara na dereva alipozinduka na kujaribu kulirejesha kwa haraka, lilipoteza mwelekeo na hatimaye kupinduka, na kusababisha vifo na uharibifu wa gari,” amesema Kamanda.
Kamanda Jongo amewashauri madereva kuhakikisha wanazingatia viwango vya usalama barabarani na kupumzika vya kutosha, kabla ya safari ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.