Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru wakazi tisa wa Ifakara, mkoani Morogoro waliokuwa wanakabiliwa mashtaka ya kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine na kujipatia Sh2.8 milioni kwa njia ya udanganyifu, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Jumatatu Julai 21,2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
Walioachiwa huru na mahakama hiyo ni Juma Mongeli(43), Abdulrahman Likenji(23), Christopher Lyuma(22), Erick Mayemba(21), Edgar Mayemba(23), Dennis Katondo(22), Emmanuel Kayega(27), Venance Makoye(29) na Jofrey Kajiru(25), wote wakazi wa Ifakara mkoani Morogoro.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya hakimu kutoa uamuzi huo, washtakiwa hao wakiwa ndani ya chumba cha Mahakama walimshukuru hakimu kwa kuweka mikono kifuani huku wakiinamisha kichwa kuashiria kushukuru.
“Asante sana Mheshimiwa, asante mno mheshimiwa,” walisikika washtakiwa hao wakishukuru huku wakiachia tabasamu na kuonyesha meno yao.
Hali hiyo ilikuwa tofauti na wakati wanapelekwa mahakamani kwani walikuwa wamekunja sura zao huku wengine wakifunika nyuso zao kwa kutumia madaftari ili wasipigwe picha, lakini baada ya mahakama kuwaachia huru, walitoka mahakamani wakiwa na nyuso za furaha huku wakinyoosha vidole viwili juu.
Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano ambayo ni kuongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh2.8 milioni kwa njia ya udanganyifu, kukutwa na kifaa kisicho halali chenye programu maalumu inayoitwa ‘miracle box software’ kwa ajili ya kubadili IMEI za simu.
Mashtaka mengine ni kusambaza ujumbe wenye maneno ‘ile hela tuma kwenye namba hii’, kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine bila kutoa taarifa TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania); kujipatia fedha kiasi cha Sh2.8 milioni kwa njia ya udanganyifu kwa kuwadanganya watumiaji wa simu kuwa kuna pesa zimetumwa kimakosa kwenye akaunti zao na hivyo wanatakiwa wazirudishe pamoja na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.
Hakimu Mwankuga alisema mahakama imepitia ushahidi wa mashahidi 13 na vielelezo 18 vilivyotolewa na upande wa mashtaka.
Pia imepitia ushahidi wa utetezi uliotolewa na washtakiwa baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.
Alisema mahakama imeangalia sheria ya upekuzi na ukamataji wa vielelezo kama ilizingatiwa wakati wa hatua hiyo.
Pia mahakama hiyo imeangalia kama vielelezo hivyo vilitunzwa kwa kufuata sheria kutoka kwa shahidi namba nane (aliyechunguza simu hizo) na mashahidi wengine kutoka kampuni za simu hapa nchini.
“Baada ya kupitia mashahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapa pamoja na utetezi wa washtakiwa, Mahakama imeona hakukuwa na ushahidi ulioonyesha utaratibu ulifuatwa wakati wa utunzwaji wa vielelezo tangu vilivyopokelewa siku ya tukio hadi vilipowasilishwa mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi,” amesema Hakimu Mwankuga na kuongeza.
“Pia mashahidi waliohusika katika ukamataji na wale waliohusika katika upekuzi nyumbani kwa washtakiwa hawakufuata sheria, kwani sheria inawataka wakati wa kufanya upekuzi lazima awepo shahidi huru, sasa katika zoezi hili, hakukuwa na shahidi huru ambaye alishiriki katika upekuzi,” amefafanua Hakimu.
Mwankuga alisema, shahidi wa saba katika kesi hiyo, Kaimu Chaurembo ambaye alitajwa na upande wa mashtaka kama shahidi huru katika kesi hiyo, hakuwa sehemu ya timu iliyokwenda kufanya upekuzi katika nyumba za baadhi ya washtakiwa.
“Pia upekuzi ulifanyika usiku na sheria inataka upekuzi huo upate ridhaa ya Mahakama, jambo ambalo halikufanywa” alisema Hakimu Mwankuga na kuongeza.
“Kwa mapungufu haya yaliyoonekana yananipa mashaka na kuwapa faida ya kuwaachia huru washtakiwa wote tisa, hivyo mahakama hii inawaachia huru washtakiwa wote” alisema Hakimu Mwakuga.
Mwakuga alisema haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo upande wa mashtaka haujaridhika na uamuzi uliotolewa.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Januari 2021 hadi Juni 2022, eneo la Ifakara wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu kwa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu, kinyume cha sheria.
Shtaka la pili, mshtakiwa Venance Makoye alikutwa na kifaa kisicho halali kwenye kompyuta yake chenye programu maalumu inayoitwa ‘miracle box software’ kwa ajili ya kubadili IMEI za simu.
Pia, wanashtakiwa wote wanadaiwa kusambaza ujumbe wenye maneno ‘ile hela tuma kwenye namba hii’ na kufanikiwa kutapeli watumiaji mbalimbali wa simu za mkononi na kujipatia pesa.