Winga teleza azitia vitani Pamba Jiji, Mtibwa Sugar

Mtibwa Sugar imeingilia dili la kumpata winga mshambuliaji wa Kagera Sugar, Erick Mwijage, baada ya nyota huyo kufikia makubaliano ya masilahi binafsi ya kujiunga na Pamba Jiji ya jijini Mwanza, kabla ya waajiri wake kuweka ngumu.

Nyota huyo alifikia makubaliano ya kujiunga na Pamba kwa mkataba wa mwaka mmoja, ingawa nyota huyo alikuwa na kandarasi ya mwaka mmoja uliobakia na Kagera iliyoshuka daraja, jambo lililosababisha Mtibwa kuingilia kati kuiwinda saini yake.

Kigogo mmoja wa Pamba alilidokeza Mwanaspoti walifikia makubaliano binafsi na nyota huyo baada ya kuwaambia yupo huru, ingawa, ghafla walipokea barua kutoka Kagera iliyowataka kukaa mezani kukubaliana, jambo ambalo limeibua sintofahamu.

“Wachezaji wetu kuna muda wanashindwa kuheshimu mikataba wanayoingia, kwa mfano anakwambia hana mkataba na unamsainisha tena mwingine kumbe hajamaliza wa mwanzoni, inasikitisha sana ila wanahitaji elimu ya kujitambua,” alisema kigogo huyo.

Kigogo huyo aliongeza bado hawajakata tamaa na wanaendelea na mazungumzo na viongozi wa Kagera kuona ni jinsi gani kwa sasa wanaipata saini ya nyota huyo, japo imewasikitisha baada ya kufikiria wamemalizana naye kumbe wanaanza tena upya.

Wakati kiongozi huyo akisema hayo, ila Mwanaspoti limepenyezewa taarifa Mtibwa na Kagera ambazo zina ushirikiano mkubwa wa kibiashara, zimekubaliana kufanya biashara, japo kilichobakia ni suala la masilahi binafsi kati ya mchezaji na klabu.

Nyota huyo aliitumikia Kagera iliyoshuka daraja msimu wa 2024-2025, ikimaliza nafasi ya 15 katika Ligi Kuu na pointi 23, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, huku akizichezea pia Geita Gold na West Armenia ya Armenia.