Zubery Katwila awindwa Coastal Union

UONGOZI wa Coastal Union, umeanza mazungumzo ya kuipata saini ya aliyekuwa Kocha wa Bigman FC, Zubery Katwila kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho msimu ujao, akienda kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Juma Mwambusi aliyeondoka.

Mwambusi aliyezifundisha Mbeya City, Yanga na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars, aliyejiunga rasmi na Coastal Oktoba 23, 2024, akichukua nafasi ya Mkenya David Ouma aliyeachana nayo Agosti 24, 2024, kwa makubaliano ya pande mbili.

Hata hivyo, licha ya Mwambusi kupewa jukumu hilo, ila aliondoka Aprili 6, 2025, kwa makubaliano ya pande mbili na ndipo uongozi ukampa kocha msaidizi, Joseph Lazaro kumalizia msimu wa 2024-2025, ingawa kwa sasa inampigia mahesabu Katwila.

Taarifa kutoka katika timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti, Katwila ni chaguo la kwanza la kikosi hicho msimu ujao, japo hakuna makubaliano rasmi yaliyofanyika hadi sasa, kutokana na kocha huyo kuwindwa na klabu mbalimbali zinazomhitaji.

“Ni mazungumzo tu ambayo hata hivyo, hayajafikia muafaka kama tunavyohitaji, suala la masilahi binafsi linajadiliwa na likikamilika pia tunaweza tukamtangaza akawa kocha wetu kwa msimu ujao wa mashindano mbalimbali,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu suala hilo, Katwila alisema yupo likizo baada ya msimu kumalizika, ingawa kukiwa na taarifa zozote juu ya sehemu au timu atakayoenda, mashabiki zake watafahamu, kwa sababu ni mapema sana kuweka wazi.

Kocha huyo mzoefu aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mtibwa Sugar, alijiunga na Bigman akichukua nafasi ya Fredy Felix ‘Minziro’, aliyejiunga na Pamba kuchukua mikoba ya Goran Kopunovic.

Akiwa na timu hiyo zamani iliyofahamika kama Mwadui FC, katika mechi 30, ilizocheza katika Ligi ya Championship msimu wa 2024-2025, alishinda 12, sare 11 na kupoteza saba, ikifunga mabao 29 na kuruhusu 21, ikiwa nafasi ya nane na pointi 47.