Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kukamata boti aina ya fibre, rangi nyeupe, iliyokuwa ikisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini Kenya kupitia Bahari ya Hindi.
Tukio hilo limetokea usiku wa Julai 22, 2025, katika eneo la Mawe Mawili, Kijiji cha Kwale, mpakani mwa Wilaya ya Mkinga na Jiji la Tanga, kufuatia taarifa za kiintelijensia na ufuatiliaji wa karibu wa mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji haramu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, amethibitisha kuwa boti hiyo ilikamatwa na Kikosi cha Polisi Wanamaji (Marine), huku watuhumiwa wawili waliokuwa ndani ya boti hiyo wakifanikiwa kutoroka baada ya kufika karibu na fukwe.
Hata hivyo, boti na shehena ya mirungi vilikamatwa salama na vipo chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Kamanda Mchunguzi amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalum kwenye maeneo ya baharini, ambayo yamekuwa yakitumiwa na wahalifu kuvusha bidhaa haramu kutoka nchi jirani.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za mapema kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu, hasa vinavyohusiana na biashara ya dawa za kulevya.