MABOSI wa Mbeya City wanasuka kikosi hicho kimyakimya kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao wa 2025-2026 na kwa sasa wako katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa winga mshambuliaji wa Pamba Jiji, Hamad Majimengi.
Nyota huyo aliyejiunga na Pamba kwa mkopo katika dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Singida Black Stars, sio chaguo la kwanza la kikosi hicho kwa msimu ujao, hivyo kupewa nafasi ya kuzungumza na timu nyingine iliyo tayari pia kumtumia.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza viongozi wa Mbeya City wameanza mazungumzo ya kina na kambi ya mchezaji huyo kwa ajili ya kuipata saini yake msimu ujao na hadi sasa kila kitu kinaenda vizuri baina ya pande zote mbili.
Akizungumza na Mwanaspoti Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Ally Nnunduma alisema mipango ya kukisuka kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao imeanza, japo ni mapema sana kuweka wazi ni mchezaji gani wanayemuhitaji katika dirisha hili kubwa.
“Kipindi hiki ni cha kuviziana kwa sababu leo nikikuambia tunafanya mazungumzo na mchezaji fulani ambaye pia washindani wetu wanamhitaji, maana yake tunakaribisha vita zaidi, hivyo acha tufanye mambo yetu kwa umakini mkubwa,” alisema.
Majimengi ni miongoni mwa nyota wazoefu na mbali na kuzichezea Singida na Pamba ila amechezea pia, JKU ya visiwani Zanzibar, Coastal Union na Namungo, jambo linalofanya mabosi wa Mbeya City kufukuzia saini yake kutokana na ubora wake.
Mbeya City ilimaliza Ligi ya Championship ikiwa nafasi ya pili na pointi 68, baada ya kushinda mechi 20, sare minane na kupoteza miwili, nyuma ya Mtibwa Sugar iliyoibuka mabingwa wapya msimu huu, kufuatia kuibuka kidedea na pointi zake 71.
Timu hiyo inayonolewa na Malale Hamsini aliyerithi mikoba ya Salum Mayanga aliyetua Mashujaa FC, ameirejesha tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, ikianza mawindo ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao ili kuongeza ushindani.