Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani ya Kijeshi (Court Martial Appeal Court), imebariki kifungo cha miaka minne jela, kwa aliyekuwa Sajini wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mussa Sahani, aliyejipatia Sh117 milioni kwa njia za udanganyifu.
Sahani aliyekuwa na nambari za kijeshi MT 85115 akiwa kambi 831 KJ Mgulani, alijipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa maofisa wenzake, akiahidi kuwaingiza ndugu zao jeshini, huku akifahamu kuwa ni uongo.
Katika ushahidi wao mbele ya mahakama ya kijeshi, mashahidi walieleza kuwa Sajini Sahani aliwaeleza kuwa ana uhusiano na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) wa wakati huo, Jenerali Venance Mabeyo hivyo itakuwa ni rahisi kwake kufanikisha suala hilo.
Jenerali Mabeyo alistaafu wadhifa huo Juni 2022 baada ya kufikisha umri wa kustaafu na nafasi yake kuchukuliwa na Jenerali Jacob Mkunda. Mabeyo kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Hata hivyo, katika utetezi wake, alikiri kupokea fedha kutoka kwa watu mbalimbali kwa kigezo cha kuwaingiza jeshini ndugu zao, lakini akadai alikuwa anakusanya fedha hizo na kuzituma kwa Meja James Makori wa makao makuu ya JWTZ.
Katika utetezi wake huo, Sajini Sahani alidai ni meja Makori ndiye aliyemwita kupitia kwa Ofisa Utawala wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania, kepteni Mwakilama, na kumwagiza kutafuta watu ambao wana shida ya kujiunga na jeshi.
Sajini Sahani alijaribu kuingiza taarifa ya miamala ya kibenki (bank statement), kujaribu kuthibitisha kuwa fedha hizo alikuwa akizituma kwa Meja Makori, lakini nyaraka hiyo ilipingwa na ikakataliwa kupokelewa kama kielelezo na Mahakama.
Katika utetezi wake, aliyakana maelezo yake yaliyopokelewa kama kielelezo PE1 cha upande wa mashitaka, akidai aliteswa ili kutoa maelezo hayo lakini akaieleza mahakama ya kijeshi kuwa chini ya ‘dili’ hiyo alikusanya Sh117 milioni.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na kuuweka katika mizania, Mahakama hiyo ilimtia hatiani Ofisa huyo katika shitaka la 1,2,6,10 na 13 na kumuhukumu kifungo cha miaka minne jela, na kumwachia huru katika makosa 8.
Hata hivyo, hakuridhika na hukumu hiyo na kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Kijeshi, ambayo chini ya jopo la majaji watatu, Awamu Mbagwa, Hamidu Mwanga na Arnold Kirekiano, ilisikiliza rufaa hiyo Julai 14,2025.
Majaji hao katika hukumu yao waliyoitoa Julai 18, 2025 na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa mtandaoni leo Jumanne Julai 22, 2025, wamesema kutiwa kwake hatiani kulikuwa ni sahihi na kifungo cha miaka minne jela alichohukumiwa ni halali kisheria.
Ushahidi wa upande wa mashitaka katika Mahakama ya kijeshi unaeleza katika tarehe tofauti kati ya Januari 1 na Desemba 31, 2022, kwa nia ya kulaghai, alijipatia Sh117 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Ilielezwa akiwa kazini kikosi cha 831 KJ Mgulani, mrufani alijipatia fedha hizo kutoka kwa watu mbalimbali kwa kisingizio kuwa angewaingiza ndugu zao jeshini huku akifahamu ni uongo na kinyume cha mwenendo mwema jeshini.
Mashahidi hao, baadhi ni maofisa wa JWTZ, walieleza kuwa mshtakiwa aliwaeleza kuwa ana uhusiano na CDF Mabeyo na kwa sababu ya uhusiano huo, alidai itakuwa rahisi kwake kufanikisha mpango huo wa kuwaingiza ndugu zao jeshini.
Mrufani aliwaeleza CDF ana nafasi maalumu kwa waumini wa kanisa lake pale Kawe jijini Dar es Salaam, hivyo akawashawishi watoe kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya ndugu zao kupata kazi jeshini na alikuwa akitafuta vijana kwa ajili hiyo.
Kulingana na ushahidi, viwango vya fedha walivyotoa vilitofautiana kutoka mtu mmoja kwenda mwingine na fedha hizo zililipwa taslimu au kupitia miamala ya simu, na alianzisha kundi la WhatsApp alilolipa jina “Nafasi za Kwaya Kawe”.
Mrufani ilidaiwa alikuwa akilitumia kundi hilo kutoa mrejesho wa maendeleo ya mchakato huo, lakini mwisho wa siku maofisa hao walishtukia kuwa wamelaghaiwa na kulikuwa hakuna nafasi za kazi JWTZ kama alivyowaaminisha.
Hapo ndipo uchunguzi ulianza makachero wa JWTZ waliingia kazini upekuzi ulifanyika ofisini na nyumbani kwa mrufani ambapo vifaa vya kielektroniki kama simu na kompyuta mpakato vilichukuliwa kwa uchunguzi.
Mashahidi kutoka kampuni za simu ambazo laini zao zilitumika kupokea fedha kutoka kwa waathirika walitoa ushahidi na kuwasilisha nyaraka zinazoonyesha mtiririko (printout) ya fedha hizo, na zikapokelewa kortini kama kielelezo.
Kwa kuongeza, mpelelezi wa kesi hiyo, kepteni Theresia Massawe aliyekuwa shahidi namba moja, alidai mrufani alikiri mbele yake na kwa mlinzi wa amani kuwa alifanya makosa hayo, alitoa maelezo yake kama kielelezo.
Baada ya mrufani kutiwa hatiani kwa makosa matano kati ya 13, alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Kijeshi, akiegemea sababu 15 ikiwamo kwamba upande wa mashitaka ulikuwa umeshindwa kuthibitisha kesi hiyo.
Sababu nyingine ni pamoja na Mahakama ya kijeshi ilikosea kumtia hatiani kwa kuegemea upekuzi batili na pia ilikosea kupekea maelezo yake ya onyo bila kufanya kesi ndani ya kesi hata baada ya kudai hakuyatoa kwa hiari yake.
Halikadhalika alidai Mahakama ya kijeshi ilikosea kisheria kwa kupokea kama kielelezo, maelezo ya ungamo kutoka kwa mlinzi wa amani wakati shahidi huyo alishindwa kuchukua maelezo hayo kulingana na sheria na miongozo iliyopo.
Mbali na sababu hizo, alidai Mahakama hiyo ilikosea kumtia hatiani kwa kuegemea hati ya mashitaka yenye dosari, ilikosea kumuhukumu bila mkosaji mkuu kuwepo na kwamba yeye hana hatia na ilikosea kuegemea ushahidi wa vifaa vya kielektroniki.
Hata hivyo, baada ya majaji kusikiliza mawasilisho ya pande mbili, ilitupilia mbali sababu hizo za rufaa wakisema wameridhika kuwa kosa la 1,2,6 na 10 yalithibitishwa , hata baada ya kuyaondoa maelezo ya onyo ya mrufani.
Majaji hao walisema Mahakama ya kijeshi ilimtia hatiani pia kwa kosa la 13 la kufanya matendo kinyume na tabia njema na utaratibu wa vikosi vya ulinzi na wao wanaona kosa hilo lilithibitishwa na kutiwa kwake hatiani kulikuwa ni sahihi.
Hata hivyo, majaji hao walisema kifungu cha 77 cha Kanuni ya Nidhamu ya Utumishi, kinataka adhabu itolewe kwa kosa moja tu hata kama mshtakiwa anakuwa ametiwa hatiani kwa makosa zaidi ya moja kama ilivyo kwa mrufani.
Ni kutokana na msingi huo, majaji hao walitumia mamlaka yao kurekebisha mwenendo wa shauri mahakama ya kijeshi ili kusahihisha adhabu aliyopewa kwa makosa yote matano, na badala yake iwe kwa kosa la kwanza pekee.