Dar es Salaam. Je, unafahamu kwamba upweke huathiri afya na ustawi wa mtu na unaweza kusababisha madhara ikiwemo kifo? Je, unajua mtu mmoja kati ya sita duniani kote anapambana na upweke? Ndio. Upweke ni halisia, utafiti umebainisha.
Upweke ni hali ya huzuni na hisia ya kutoridhika inayotokana na kujihisi uko peke yako kinyume na vile unavyohitaji, kama anavyosema mkurugenzi wa kituo cha kushughulikia upweke katika Chuo Kikuu cha Sheffield Hallam nchini Uingereza, Dk Andrea Wickfield.
Wataalamu wengi wanakubali kwamba upweke hutokea unapohisi hali ya uhusiano wako binafsi na watu wengine uko chini kuliko vile unavyotamani uwe, jambo linalosababisha ujihisi huna thamani.
Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni wa Chuo Kikuu cha Cambridge umegundua kwamba hisia za upweke zinahusishwa na hatari kubwa ya ugonjwa wa moyo. Pia, huongeza hatari ya kiharusi na kisukari cha aina ya pili.
Dk Wickfield anasema wanasayansi wamepata ushahidi kwamba upweke husababisha shida ya akili, unyonge na wasiwasi na huongeza hatari ya kifo.
Sababu hasa ya uhusiano huo bado haijulikani, lakini madaktari wanaeleza upweke unaweza kusababisha msongo wa mawazo wa ndani. Upweke wa muda mrefu unaunyima ubongo vichocheo vinavyoathiri michakato ya fikra na hilo linaweza kuzidisha matatizo ya afya ya akili.
Ripoti ya kimataifa ya Tume ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya Uunganisho wa Kijamii iliyotoka Juni 30, 2025 inaeleza mtu mmoja kati ya sita duniani kote ameathiriwa na upweke. Upweke unahusishwa na takriban vifo 100 kila saa, zaidi ya vifo 871,000 kila mwaka.
Ni vizuri kutaka kuwa peke yako nyakati nyingine, lakini inapofikia hatua hiyo ndio mtindo wa maisha yako ya kila siku ni hatari. Kujihisi mpweke ni kitu kibaya kiafya kwani huchangia kushusha kinga za mwili.
Mwenyekiti mwenza wa Tume hiyo ya WHO na Balozi wa afya wa zamani wa Marekani, Dk Vivek Murthy amesema katika ripoti hiyo wamebainisha kwamba upweke na kutengwa kama changamoto kuu katika wakati wa sasa.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amesema kwa sasa watu wengi wamejikuta wakitengwa na wakiwa wapweke ambapo mbali na athari kwa watu binafsi, familia na jamii, bila kushughulikiwa, upweke na kutengwa vitaendelea kugharimu jamii mabilioni kwa gharama za huduma za afya, elimu na ajira.
Akinukuliwa kwenye makala ya Mwananchi Mei 2, 2025, mtaalamu wa saikolojia tiba na afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Isaac Lema alisema upweke ni tatizo linalopaswa kuepukwa, japo kuwa peke yako si tatizo.
Dk Lema alisema mtu mpweke hata ukimweka katikati ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, bado atajiona yuko katika hali ya upweke kwa sababu amekosa mjumuiko na watu wengine hata kama kuna watu wanaomzunguka.
Akizungumza leo na Mwananchi, mtaalamu wa tiba, Dk Fabian Maricha anasema upweke unatokana na changamoto ya afya ya kiakili pale mtu anapojitenga na kuwa peke yake ikiwamo katika utatuzi wa matatizo yake.
“Mtu akikata tamaa ya maisha ndiyo unasikia mtu amekunywa sumu, kujinyonga au kujiua kwa namna yoyote ile. Anakuwa anajihisi hana thamani, hamna mtu anayejali, ndio anaona bora ajiondoe uhai wake,” amesema Dk Maricha.

Amesema cha kufanywa hapo ni kusaidia watu wenye changamoto ya namna hii ikiwemo kuwafanya wajichanganye na watu wa makundi mbalimbali ili aweze kufahamu kwamba si pekee wenye shida ya namna hiyo, lakini pia kuwatafutia madaktari, washauri, watu wa ustawi wa jamii na wanasaikolojia.
WHO imeeleza upweke unaathiri watu wa rika zote, hasa vijana na watu wanaoishi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati (LMIC). Kati ya asilimia 17-21 ya watu wenye umri wa miaka 13-29 waliripoti kuhisi upweke huku viwango vya juu zaidi vikiwa miongoni mwa vijana.
Takriban asilimia 24 ya watu katika nchi zenye kipato cha chini waliripoti kuhisi upweke mara mbili zaidi ukilinganisha na nchi zenye kipato cha juu (takriban asilimia 11).
Mwenyekiti mwenza wa Tume ya WHO ya Uunganisho wa Kijamii na Mshauri wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Chido Mpemba amesema hata katika ulimwengu huu wa kidijitali, vijana wengi wanahisi upweke.
“Kadiri teknolojia inavyoleta upya katika maisha yetu, lazima tuhakikishe inaimarisha sio kudhoofisha uhusiano wa kibinadamu,” amesema.
Vilevile, kutengwa kijamii inakadiriwa kuathiri hadi mtu mmoja kati ya watu wazima watatu na mtu mmoja kati ya vijana wanne.
Inaelezwa kuwa upweke na kutengwa na jamii kuna sababu nyingi ikiwa ni pamoja na afya duni, kipato cha chini, ukosefu wa elimu, kuishi pekee, miundombinu isiyotosheleza ya kijamii na sera za umma na teknolojia za kidijitali.
Mwisho, ripoti hiyo imeeleza suluhu la kupunguza upweke na kutengwa kijamii lipo katika ngazi za kitaifa, jamii na mtu binafsi na zinatoka katika kuongeza uelewa na kubadilisha sera za kitaifa hadi kuimarisha miundombinu ya kijamii (mfano bustani, maktaba, migahawa) na urahisi wa kufikia saikolojia.
Dk Daud Emmanuel, daktari wa binadamu kutoka Zanzibar anasema ni kweli upweke na kujitenga na jamii husababisha vifo vya mapema.
Akielezea kiundani amesema akianza na sonona na mawazo ya kujinyonga anasema watu wengi wanapokuwa wapweke uwezo wao wa kufikiria kwa umakini hupungua na hivyo kufanya uamuzi hata ya kujiondoa uhai wao wenyewe.
“Na wakati wanafanya uamuzi huo hujiona wako sahihi maana akili huwa zimefikia mwisho wa kutafakari.
“Mtu mwenye upweke huwa na tabia hasi za kiafya, kama tabia za kunywa pombe kupita kiasi, uvutaji sigara, kuwa na ulaji usiofaa kiafya, kutofanya mazoezi na matumizi ya dawa za kulevya, hugeukia tabia hizi ili kuziba pengo la uhusiano usioridhisha kati yake na jamii inayomzunguka,” amesema.
Amesema tabia hizo hasi za kiafya huwa ni sababu ya maradhi mengi yasioambukizwa kama vile saratani, sukari, shinikizo la damu, maradhi ya ini na hatimaye huishia kupoteza maisha.
Dk Emmanuel anasema upweke hushusha kinga ya mwili moja kwa moja kwani wakati ukiwa na msongo wa mawazo, mambo kadhaa hutokea kwenye mwili kama vile kutolewa kwa wingi vichecheo aina ya cortisol ambayo husababisha shinikizo la damu na baadaye kiharusi.
“Pia, kichocheo cortisol baadaye husababisha kushusha kinga ya mwili na hivyo kupunguza uwezo wa mwili kupambana na maradhi ambukizi. Pia, vichocheo vinavyotolewa kipindi cha msongo kama cortisol hupandisha sukari mwilini na hali hii ikidumu kwa muda mrefu husababisha kisukari,” amefafanua.