INEC yatilia mkazo wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia sheria

Pemba. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imewataka waratibu na wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyotolewa na Tume hiyo katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia shughuli za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Wito huo umetolewa leo Julai 22, 2025  na Makamu Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mbarouk Salum Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waratibu wa uchaguzi, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa ngazi za majimbo kanda ya Pemba yaliyofanyika ukumbi wa Makonyo Wawi Chakechake.

Amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria zinazopaswa kufuatwa ili kuimarisha utendaji kazi jambo litakaloweza kusaidia   kuifanya shughuli hiyo kwa wepesi.

“Jukumu la kusimamia uchaguzi ni kubwa hivyo wasimamizi mnapaswa kuwa makini kwa  kufuata maelekezo ya misingi ya sheria na mafunzo mnayopewa katika kusimamia mchakato huu,” amesema.

Aidha, amewataka wasimamizi na waratibu hao kujiepusha na migogoro na kuwa chanzo cha malalamiko kwa kujihusisha na ushabiki wa chama cha siasa kwani jambo hilo linaweza kuathiri hatua hiyo.

“Niwaombe waratibu na wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanafuata misingi ya sheria na maelekezo yanayotolewa na INEC tumetoa mafunzo haya kwa ajili kwenda kusimamia zoezi hili kwa misingi  inayokubalika,’’ amesema Jaji.

Amewataka kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu katika hatua mbalimbali, huku akiwasisitiza  kujiepusha na ushabiki wa kisiasa na kuacha upendeleo wa aina yoyote katika utoaji wa ajira kwa watendaji wa tume.

Aidha, amewataka kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema na kutoa taarifa kwa wadau, pamoja na kutoa taarifa za kuapishwa kwa mawakala kwa vyama vyote kwa wakati na mahala sahihi palipopangwa kufanyika shughuli hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa INEC,  Adam Mkina amewaomba waratibu na wasimamizi kutekeleza majukumu yao kwa usiri wakizingatia Katiba, sheria na Kanuni na viapo walivyokula.

Awali, akizungumza baada ya kuwaapisha, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Chakechake, Nassor Suleiman Nassor amewataka kuzingatia  uadilifu katika kutekeleza majukumu yao.