Arusha. Jaji Gabriel Malata wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, anayesikiliza rufaa ya mirathi iliyokatwa na Angela Mathayo, ametupilia mbali maombi ya kutaka ajitoe kusikiliza rufaa hiyo kwa kile alichodai hayana mashiko kisheria.
Katika maombi hayo ndani ya rufaa, yaliyowasilishwa Machi 12, 2025 na wakili wa Anjela ambaye aliieleza mahakama hiyo kuwa alipokea maelezo kutoka kwa mteja wake wakimtaka Jaji ajiondoe ambapo walikuwa na sababu mbili.
Wakili Joseph Bitakwate, anayemwakilisha Angela katika rufaa hiyo alieleza kuwa mteja wake amemtaka awasilishe hoja ya Jaji kujiondoa kusikiliza rufaa hiyo iliyotokana na shauri namba 10/2023 katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba.
Wakili huyo alitaja sababu kuwa ni Jaji aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo kushauri pande zote mbili kujaribu kusuluhisha suala hilo nje ya mahakama jambo lililomfanya mrufani kutokuwa na imani naye.
Mgogoro alioshauri Jaji usuluhishwe nje ya mahakama ni unaomuhusisha mrufani, mama na watoto wake kufuatia ugawaji wa mali za marehemu Felix Bakuza (baba wa watoto hao).
Sababu ya pili ni Jaji aliibua mwenyewe hoja kuhusu ustahimilivu wa rufaa na mwenendo (wa shauri) katika Mahakama ya chini unaomgusa mdaiwa (Serikali) na haki ya kisheria ya mdaiwa baada ya kuwa amegawanya mali za marehemu hoja ambayo bado haijazungumzwa.
Jaji huyo ametoa uamuzi huo Julai 18,2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama ambapo amesema suala ambalo mahakama italiangalia ni kuzingatia kanuni za Jaji au Hakimu kujitoa katika kesi.
Amesema suala la kujitoa kwa Jaji au Hakimu haliongozwi na hisia za mtu bali kanuni za kisheria ikiwemo kutopendelea upande mmoja au kuwa na mgongano wa kimasilahi ikiwemo wa kifamilia, ambao unaweza kuathiri uamuzi wa mahakama.
Jaji huyo amesema Wakili Joseph aliieleza mahakama kwamba aliagizwa na mteja wake kufikisha ujumbe Jaji ajitoe, na mahakama imechukua muda kusoma maelezo ya wakili huyo na kuwa hakuna kilichowekwa wazi kuwa kuna upendeleo.
Jaji huyo amesema Wakili huyo anafahamu mazingira yanayoweza kusababisha kukataliwa kwa Jaji au Hakimu kuendesha kesi na kutokana na kukosekana kwa sababu hizo, wakili huyo alipaswa kumuongoza mteja wake ipasavyo.
Ameongeza kuwa wakili ana wajibu kwa Mahakama, mteja, mashahidi na umma kabla ya kufikisha alichoelekezwa na mteja, kama ni halali kisheria na kuwa hapaswi kuwasilisha maagizo yasiyokubalika kisheria.
“Mteja anaweza kuagiza chochote lakini ni wajibu wake kumshauri ipasavyo ,kwani siyo yote yanayosemwa na mteja au kuelekezwa yanakubalika kisheria, ni jukumu la wakili kumshauri mteja ipasavyo,”amesema Jaji
Jaji huyo amesema kushauri au kuhimiza utatuzi mbadala wa migogoro ni mojawapo ya vipengele muhimu katika utatuzi wa migogoro na hiyo inaweza kufanyika katika hatua yoyote.
“Hayo yameelekezwa katika Ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.”
Amesema kwa mujibu wa kifungu hapo juu, ni wazi kwamba, Mahakama zimepewa jukumu la kuongeza matumizi ya masuluhisho mbadala katika kutatua migogoro.
Jaji amesema mbali na ibara hiyo kanuni za 58 na 59 za Kanuni za Mawakili (Mwenendo na Maadili ya Kitaalamu) za 2018 zinaweka wajibu kwa mawakili.
“Kwa yote ambayo yamesemwa Mahakama hii inashikilia kuwa, mrufani kupitia Wakili Joseph, ameshindwa kutoa maelezo ya kuwepo kwa sababu za kutenguliwa/kutenguliwa kwa Jaji,”amehitimisha
Awali Wakili huyo alidai kuwa mteja wake amepoteza imani kwa Jaji na kwamba haki haitaonekana kutendeka katika mazingira hayo.
Amesema kuwa mteja wake hakufurahishwa na maneno yaliyotolewa na mahakama hiyo Februari 18,2025 ya kuwashauri wahusika kujaribu kutafuta suluhu nje ya mahakama kwa kuwa mirathi ilishagawanywa kwa walengwa.
Aidha mahakama ilishauri wahusika kukubaliana, pamoja na mambo mengine kuwa, watoto wa mrufani kujenga nyumba nyingine kwenye ardhi iliyogawiwa kwa mrufani, badala yake kupigania nyumba tajwa ambayo tayari imegawanywa na mrufani na watoto wake.
Mahakama ilifafanua kuwa mrufani alipewa chumba kimoja lakini yeye alitaka nyumba nzima hivyo watoto wanaweza kujenga nyumba nyingine katika eneo lililogawanywa kwa mrufani.
Zaidi ya hayo, alidai kuwa, mahakama hii ilimshauri mrufani kuwa, gharama za uendeshaji wa kesi hiyo zinaweza kutumika kujenga nyumba nyingine katika ardhi hiyo, hali iliyosababisha mrufani kupoteza imani na Jaji na kuomba ajitoe.